Bunge la Algeria lakosoa siasa za kinafiki za nchi za Magharibi
Bunge la Algeria limeyalaumu mabunge ya nchi za Magharibi kwa siasa zao za kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na maandamano na machafuko ya hivi karibuni nchini Ufaransa.
Wimbi la hasira na ghadhabu za wananchi limeenea kote nchini Ufaransa baada ya polisi wa nchi hiyo kumuua kwa kumpiga risasi Nahel Marzouq aliyekuwa na umri wa miaka 17 Jumanne wiki iliyopita katika kitongoji cha Nanterre huko Paris. Kutokana na mauaji ya kijana huyo mwenye asili ya Algeria, wananchi wa Ufaransa walichoma moto magari na majengo mengi ya umma mjini Paris na katika maeneo mengine ya Ufaransa.
Maandamano na machafuko hayo yalikabiliwa kwa mkono wa chuma wa vyombo vya usalama vya Ufaransa ambapo askari usalama walitumia ukatili na silaha za moto kukabiliiana na maandamano ya wananchi.
Kufuatia hali hiyo Bunge la Algeria, limetoa taarifa likilaani mauaji yaliyofanywa na polisi ya Ufaransa dhidi ya Nahel Marzouq na kutangaza kuwa, mabunge ya nchi za Magharibi yamenyamaza kimya mbele ya mienendo ya ubaguzi wa rangi nchini Ufaransa na kwamba yamekhitari sera za kinafiki na kindumakuwili.
Akizungumzia suala hilo, Mohamed Larbi Ould Khelifa, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Algeria, amehoji madai ya nchi za Magharibi kwamba zijali maadili ya kuishi pamoja kwa amani na kuheshima mataifa mengine.
Kitendo cha afisa wa polisi wa Ufaransa kumuua Nahel Marzouq, kijana mwenye asili ya Algeria katika siku za hivi karibuni, kwa mara nyingine tena kimeigeuza Ufaransa kuwa uwanja wa machafuko na maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi.

Raia wengi wa Ufaransa wamejitokeza mitaani kupinga sera hizo, na katika siku chache zilizopita, miji mingi ya nchi hiyo imekuwa uwanja wa maandamano na makabiliano ya polisi na waandamanaji. Maandamano hayo kimsingi yameipoozesha Ufaransa na kuzifanya nchi nyingine za Ulaya kuingiwa na hofu kubwa, kwa namna ambayo Nancy Faeser, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, amekiri kwamba Waislamu wengi wa nchi hiyo wanasumbuliwa na ubaguzi na suala hili linaongeza chuki katika jamii.