Viongozi wa Afrika wajadili njia za kupunguza rushwa barani humo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar nchini Tanzania, Hemed Suleman Abdulla amezitaka nchi mbalimbali barani Afrika kushirikiana na kushikamana ili kupunguza vitendo vya rushwa barani humo.
Abdulla ametoa mwito huo leo Jumapili jijini Arusha kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa barani Afrika.
Pia yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kusainiwa mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa. Aidha maadhimisho hayo yamesadifiana na miaka 21 ya Umoja wa Afrika. Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika OAU baada ya uamuzi huo kupitishwa na viongozi wa nchi za bara hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema kuwa, nchi za Afrika zinapaswa kuungana kupambana na rushwa kwani rushwa ni adui na inaathari katika utawala bora na kukuza uchumi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Tanzania wapo tayari kushirikia kwa vitendo kupitia mkataba huo waliosaini na nchi mbalimbali katika kuhakikisha suala la mapambano dhidi ya rushwa linatokomezwa. Amesema kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni "kuendeleza uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa Barani Afrika."
Simbachawene amesema kongamano hilo litakalofanyika rasmi kesho Julai 10, litatoa fursa kwa nchi mbalimbali kupeana na kubadilishana uzoefu namna ya kupambana na rushwa katika bara la Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni amesema katika kuadhimisha siku ya kupambana na rushwa barani Afrika ambayo kilele kinatarajiwa kufanyika Julai 11, itakwenda sambamba na kongamano litakalofanyika jijini Arusha ambalo litawashirikisha wadau mbalimbali.