Iran yalaani siasa za Marekani za kuchochea vita dhidi ya Venezuela
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani tishio la Marekani la kutumia mabavu dhidi ya mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya Venezuela.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetahadharisha katika taarifa iliyotoa siku ya Alkhamisi kuhusu taathira na matokeo hatari ya chokochoko za Marekani katika amani na usalama wa eneo la Caribbean.
Taarifa hiyo inasema kuwa, hatua hizi za Marekani ambazo ni muendelezo wa uingiliaji na siasa zinazokiuka sheria za nchi hii dhidi ya taifa la Venezuela ni ukiukwaji mkubwa wa Hati ya Umoja wa Mataifa hasa kufungu cha 4 cha Ibara ya 2 inayopiga marufuku matumizi ya nguvu au vitisho dhidi ya nchi huru na ni ishara tosha ya kuongezeka ukiukaji mkubwa unaofanywa na watawala Marekani dhidi ya kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa.
Ikikumbushia kanuni za kimsingi za Hati ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuheshimiwa mamlaka za kitaifa na haki ya kujitawala mataifa, pamoja na kupigwa marufuku kutumiwa mabavu dhidi ya nchi huru, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mshikamano wake na taifa na serikali ya Jamhuri ya Venezuela na wakati huo huo kusisitiza haja ya Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kushughulikia haraka hali inayohatarisha usalama na amani katika eneo la Caribbean.