Ulimwengu wa Spoti, Jul 22
(last modified Mon, 22 Jul 2024 05:38:08 GMT )
Jul 22, 2024 05:38 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jul 22

Hujambo mpenzi msikilizaji, na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyoshuhudiwa katika kona mbalimbali za dunia ndani ya siku saba zilizopita...

Mieleka: Iran bingwa wa Asia

Timu ya taifa ya mieleka mtindo wa Greco-Roman ya vijana wenye chini ya miaka 20 imeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Mabingwa wa Asia yaliyofanyika Thailand. Kwenye mashindano hayo yaliyofunga pazia lake Jumapili, vijana wa Iran walitawazwa mabingwa kwa kuzoa medali 6 za dhahabu, 1 ya fedha na 2 za shaba.

Kabla ya hapo, timu ya mieleka ya Grec-Roman ya vijana wenye china ya miaka 15 ya Iran iliibuka mshindi wa mashindano hayo baada ya kuchota medali 3 za dhahabu, 2 za fedha na 2 za shaba.  

Olimpiki: Iran kupeleka wanariadha 66

Ujumbe wa pili wa wanariadha wa Iran waliondoka nchini Alkhamisi ya Julai 19 kwenda kushiriki Duru ya 33 ya Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024. Michezo hiyo inaanza Julai 26 na kuendelea hadi Agosti 11. Zaidi ya wanamichezo 10,500 kutoka kona mbalimbali za dunia wanatazamiwa kushiriki michezo 32.

Kundi la kwanza linalojumuisha wanamichezo 40 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran liliondoka nchini Julai 16 kwenda Paris.

Wakati huo huo, Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki ya Iran NPC itatuma wanariadha 66 kwenda kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Walemavu yam waka hu 2024 huko Paris, Ufaransa.

Mashindano hayo yanafanyika baina ya Agosti 28 na Septemba 8, ambapo wanariadha na wanamichezo zaidi ya 4,000 watachuana katika mashindano mbalimbali kuwania medali 549.

Palestina inatuma wanamichezo wanane tu kwenda kushiriki mashindano hayo ya kimataifa ya msimu wa joto kai huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa.

Raga: Zimbabwe yaibandua Uganda Kombe la Afrika

Timu ya taifa ya mchezo wa raga ya Zimbabwe imeibandua mwenyeji Uganda kwenye fainali za Kombe la Afrika zinazoendelea kuroroma mjini Kampala. Zimbabwe Sables iliizaba Uganda Rugby Cranes 22-20 katika mchezo wa robo fainali ya mashindano hayo ya kieneo ya raga, licha ya kuupigia nyumbani mbele ya maelfu ya mashabiki. Miamba ya raga Afrika, Namibia, inatazamiwa kuvaana na Zimbabwe kwenye nusu fainali ya mashindano hayo. Kenya ambayo iliiondoa Senegal kwenye robo fainali, itachuana na Algeria kwenye nusu fainali ya pili. Mwenyeji Uganda atafunga kazi na Burkina Faso, kama ambavyo Senegal itatoana udhia na Kodivaa. Fainali ya Kombe la Afrika kwenye mchezo wa raga itapigwa Julai 28.

Yanga yazabwa kiume Afrika Kusini

Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania imezabwa mabao 2-1 katika mchezo wa mashindano ya Kombe Kuu la Kimataifa la Mpumalanga dhidi ya klabu ya Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Ujerumani (Bundesliga). Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki ulifanyika kwenye uwanja wa Mbombela uliopo katika Jimbo Mpumalanga nchini Afrika Kusini. Licha ya kuzabwa, lakini Yanga wameonesha kiwango cha hali ya juu katika mechi hiyo ya kimataifa dhidi ya Augsburg ya UjerumaniTimu zote mbili zipo katika maandalizi kujiweka sawa kwa ajili msimu mpya wa mashindano. Timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo ni TS Galaxy ya Afrika Kusini na Mbabane Swallows ya Eswatini.  Wananchi wanatazamiwa kucheza mechi nyingine ya kujinoa dhidi ya klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mnamo Julai 29.

CECAFA kupandishwa hadhi

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema linataka kuyafanya mashindano ya Kombe la Dar Port Kagame kuwa makubwa zaidi kuanzia msimu ujao. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Julai 18, Rais wa CECAFA, Wallace Karia amesema baraza hilo linafanya mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusu namna gani ya kuhakikisha michuano hiyo inafanyika kwa kiwango kikubwa.

Rais wa CECAFA, Wallace Karia

Katika kuhakikisha yanapewa kipaumbe kikanda amehimiza vyama vya soka kila nchi kuyaingiza kwenye kalenda zao ili kila mwaka yawe yanafanyika kuzisaidia timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kujiweka imara.

BDS yakosoa FIFA kuikingia kifua Israel

Harakati ya Kimataifa ya Kuususia Utawala Haramu wa Israel BDS imelikosoa vikali Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa kuakhirisha kura ya kuisimamishia uanachama Israel katika taasisi hiyo kubwa zaidi ya soka duniani. Mei mwaka huu, Shirikisho la Soka Asia (AFC) lilitangaza kuunga mkono ombi la Palestina la kulitaka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) liifutie uanachama Israel katika taasisi hiyo kubwa zaidi ya kandanda duniani, kutokana na utawala huo wa Kizayuni kutenda jinai kubwa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Uungwaji mkono wa Palestina katika kona zote za dunia

Aidha Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwezi Februari mwaka huu pia liliiandikia barua FIFA likilitaka lisitishe shughuli zote za soka za utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na utawala huo kutenda jinai huko Gaza. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Palestina, mamia ya wachezaji wa Kipalestina wameuawa shahidi na kujeruhiwa, pamoja na kubomolewa kwa viwanja vya soka huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, tangu kuanza kwa vita vya Gaza Oktoba 7, 2023, vilivyoua Wapalestina zaidi ya 39,000.

……………….TAMATI…………..