Alfajiri Kumi- Sekta ya afya ya Iran kabla na baada ya Mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/event-i136294-alfajiri_kumi_sekta_ya_afya_ya_iran_kabla_na_baada_ya_mapinduzi
Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya vipindi maalumu vinavyokujieni kwa mnasaba wa siku hizi za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kipindi chetu kinazungumzia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya afya na ustawi wa jamii.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Feb 05, 2026 14:50 UTC
  • Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu
    Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya vipindi maalumu vinavyokujieni kwa mnasaba wa siku hizi za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kipindi chetu kinazungumzia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya afya na ustawi wa jamii.

Afya na ustawi wa jamii ni miongoni mwa mambo yanayohusiana moja kwa moja na maisha, hadhi na ubora wa maisha ya watu. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo yaliyoanza kwa kauli mbiu ya kupigania uadilifu na utu wa binadamu hayangeweza kubaki hivi hivi bila kujali afya ya miili na maisha ya watu. Kipindi hiki kinasimulia safari ambayo imeitoa Iran kwenye mfumo wa huduma za afya za kimatabaka na kibaguzi wa kabla ya Mapinduzi, hadi kwenye mojawapo ya mitandao mipana zaidi ya huduma za afya katika eneo la Magharibi mwa Asia. Ni njia ambayo imekuwa na changamoto, gharama kubwa, lakini wakati huo huo yenye heshima na fahari kubwa.    ****

Ili kuelewa kwa kina mabadiliko yaliyotokea katika sekta hii, ni lazima turudi nyuma kwenye miaka ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu. Katika miaka ya 1340 na 1350 Hijria Shamsia, mfumo wa afya wa Iran haukuwa na usawa na uadilifu bali ulitawaliwa na ubaguzi. Katika miji mikubwa, hasa Tehran, kulikuwa na hospitali zenye vifaa vya kutosha na madaktari walioelimishwa katika nchi za Magharibi. Lakini suhula hizi zilihudumia kundi la matajiri wachache na watu waliokuwa karibu na utawala wa kifalme. Kwa upande mwingine, watu wengi, hasa wakazi wa vijiji na maeneo ya watu maskini, walinyimwa huduma za msingi za afya. Maelfu ya vijiji havikuwa hata na kituo cha afya au daktari. Magonjwa rahisi ya kuambukiza, utapiamlo na vifo vingi vya watoto wachanga na wajawazito viliakisi hali mbaya ya maisha katika sehemu kubwa ya Iran ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Matarajio ya umri wa kuishi katika miaka ya 1970 yalikadiriwa kuwa takriban miaka 55, takwimu iliyoonyesha udhaifu mkubwa katika mfumo wa afya na ustawi wa jamii.

Wakati huo, huduma ya afya ilizingatiwa zaidi kama "jambo la anasa" na si "haki ya umma." Gharama za matibabu zilikuwa kubwa mno, na familia nyingi ziliepuka kwenda kumuona daktari kutokana na umaskini. Bima ya afya ilikuwa ya kundi dogo sana la watu, haikuwa na ufanisi, na haikutoa huduma pana. Serikali ilikuwa na mchango mdogo katika kutoa huduma za afya ya umma, na mbinu kuu ilikuwa kuagiza dawa na huduma za matibabu kutoka nje ya nchi. Si hayo tu, bali hata sehemu kubwa ya madaktari bingwa walikuwa wageni, na utegemezi wa kisayansi na kivitendo katika uwanja huu ulikuwa dhahiri. Mapinduzi ya Kiislamu yaliona hali hii si tu kama tatizo la usimamizi, bali pia kama dhulma ya kitaasisi. Kwa hivyo, afya ya watu, kama mojawapo ya nguzo za uadilifu wa kijamii, ilipewa kipaumbele katika kubuni sera za mfumo mpya.

Mojawapo ya hatua za kwanza na muhimu zaidi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ilikuwa kustawisha mtandao wa huduma ya afya ya msingi. Yumkini hatua hii ikawa haionekana sana, lakini imekuwa na athari kubwa kwa afya ya umma. Katika miaka ya 1980, sambamba na hali ngumu ya vita vya kulazimishwa na ukosefu wa rasilimali, Iran iliamua kujikita kwenye kinga na huduma ya afya ya msingi badala ya kuzingatia hospitali kubwa za mijini pekee. Matokeo ya uamuzi huu yalikuwa kuanzishwa mtandao mkubwa wa vituo vya afya katika vijiji na maeneo ya watu maskini. Vituo vya afya, vilivyoongozwa na "wafanyakazi wa afya" wa eneo husika, vilitoa huduma za msingi kama vile chanjo, huduma kwa akina mama wajawazito, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, na kutoa elimu ya afya na lishe. Mbinu hii ilifanikiwa sana kiasi kwamba baadaye ilitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mojawapo ya mifano bora ya kutoa huduma za afya ya msingi.

Kupanuliwa kwa mtandao huo kuliandamana na matokeo ya kustaajabisha. Vifo vya watoto wachanga na watoto vilipungua sana na magonjwa ya kuambukiza kama vile polio, surua na pepopunda ya watoto wachanga, ambayo yalikuwa tishio kubwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yalidhibitiwa au kukomeshwa kabisa katika baadhi ya maeneo. Operesheni za kutoa chanjo kote nchini ilikuwa jambo la kawaida, hata katika sehemu za mbali zaidi nchini. Mafanikio haya yalipatikana wakati nchi ikiwa katika vita kubwa kwa wakati mmoja. Lakini mtazamo wa Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa kwamba, afya za wananchi hazipaswi kutolewa kafara hata katika hali na vipindi vigumu zaidi. Huu ndiyo uhusiano wa kina kati ya "kulinda mipaka" ya nchi na "kulinda maisha ya watu."

Sambamba na huduma ya afya ya msingi, upanuzi wa miundombinu ya huduma ya afya pia uliendelea kwa kasi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mamia ya hospitali, kliniki na vituo maalumu vya afya vilijengwa au kupanuliwa kote nchini. Vyuo vikuu vya matibabu vilianzishwa katika makao makuu ya mikoa na hata wilaya nyingi ili kutoa mafunzo kwa rasilimali watu yenye utaalamu, huku huduma za matibabu zikiendelea. Hii leo, karibu hakuna eneo lolote nchini Iran ambalo halina huduma zinazofaa za afya. Idadi ya vitanda vya hospitali imeongezeka, na taaluma za matibabu za madaktari bingwa ambazo zilikuwa chache sana kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu sasa zinafundishwa kwa kiwango kikubwa ndani ya Iran. Maendeleo haya yameondoa utegemezi wa Iran kwa madaktari wa kigeni na yameiwezesha nchi kujitegemea katika nyanja zote za tiba bali hata kuwa kituo kikuu cha utalii wa kitiba katika eneo la Magharibi mwa Asia.      **********

Mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu katika uwanja wa afya ni maendeleo katika uzalishaji wa dawa na chanjo. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, dawa nyingi zilizotumiwa nchini ziliagizwa kutoka nje, na viwanda vya dawa vya ndani vilikuwa vichache sana na tegemezi kwa nchi za Magharibi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hasa katika miaka ya 1990 na 2000, uwekezaji mkubwa ulifanywa katika uwanja huo. Leo, zaidi ya asilimia 95 ya dawa zinazotumiwa nchini Iran zinazalishwa ndani ya nchi. Iran imepata nafasi muhimu katika uzalishaji wa dawa tata, dawa za bioteknolojia, dawa za kupambana na saratani na dawa za wagonjwa maalumu. Kujitosheleza huku kulithibitika kuwa muhimu sana katika kipindi cha vikwazo vikali, ambapo maadui walifanya jitihada za kulenga afya ya watu wa Iran kwa kuweka vikwazo vya dawa, lakini uwezo wa ndani ya nchi ulizuia janga la binadamu.

Mfano wa wazi wa uwezo huu ulikuwa wakati wa janga la COVID-19. Wakati nchi nyingi zinazoendelea zilipokuwa tegemezi sana kwa madola makubwa duniani kwa ajili ya kupata chanjo na vifaa vya matibabu ya janga hilo, Iran iliweza kutengeneza chanjo kadhaa za ndani kwa kutegemea wanasayansi wake. Wakati huo huo, uzalishaji mkubwa wa barakoa, mashine za kupumulia, vifaa vya uchunguzi, na dawa muhimu ulifanyika ndani ya Iran. Uzoefu huu kwa mara nyingine ulionyesha kwamba uhuru na kujitawala kisayansi na viwanda unahusiana moja kwa moja na afya ya watu. 

Pamoja na haya yote inatupasa kusema kuwa, huduma ya afya ni sehemu tu ya dhana pana ya ustawi wa jamii. Tangu mwanzoni kabisa, Mapinduzi ya Kiislamu yalijitolea kusaidia makundi yaliyo katika mazingira magumu. Kubuni na kuanzishwa taasisi kama vile Kamati ya Msaada ya Imam Khomeini, Shirika la Ustawi wa Jamii, na upanuzi wa bima ya jamii kulikuwa katika mwelekeo huu. Taasisi hizi zilianza shughuli zao kwa lengo la kusaidia familia zilizohitaji msaada, watu wenye ulemavu, wazee, wanawake wanaotunza kaya na watoto wasio na walezi. Mamilioni ya watu wamefaidika na misaada, pensheni, nyumba, ajira na huduma za uwezeshaji za taasisi hizi katika miongo minne iliyopita.

Kumekuwapo maendeleo makubwa pia katika sekta ya bima. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, watu waliokuwa na bima ya afya walikuwa wachache sana na sehemu kubwa ya jamii, hasa wakazi wa vijijini na wafanyakazi wasio rasmi, walinyimwa bima yoyote ya afya au pensheni. Leo, na kutokana na kupanuliwa bima ya hifadhi ya jamii, huduma za matibabu, afya na bima kwa wanakijiji na wahamaji, asilimia kubwa ya jamii nchini inafaidika na bima. Mipango kama vile bima ya afya kwa wote imekuwa ikitekelezwa kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu na kuzuia watu kuwa maskini kutokana na magonjwa. Ingawa mipango hii imekabiliwa na changamoto kama vile upungufu wa rasilimali na usimamizi wa fedha, lakini harakati ya kuelekea kwenye huduma bora ya afya kwa wote inatambuliwa kuwa mafanikio muhimu ya kijamii.

Matokeo ya sera na hatua hizi zote yanaonekana wazi katika viashiria vya afya vya jumla. Umri wa kuishi nchini Iran umeongezeka kutoka takriban miaka 55 katika miaka ya 1970 hadi takriban miaka 77 katika miaka ya hivi karibuni. Vifo vya watoto wachanga vimepungua sana, na Iran imekaribia kiwango cha nchi zilizoendelea katika viashiria vingi vya afya. Upatikanaji wa maji salama ya kunywa, lishe bora, kuengezeka uelewa wa masuala ya afya, na kupanuliwa huduma za afya ya umma, yote yamechangia katika mafanikio haya. Nambari hizi  si takwimu tu, bali kila nambari ni sumulizi ya kuokoa maisha.

Hapana shaka kwamba, njia ya afya na ustawi wa jamii baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu imekabiliwa na changamoto nyingi. Ukuaji wa idadi ya watu, mabadiliko ya magonjwa kutoka magonjwa ya kuambukiza hadi magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo na saratani, kupanda kwa gharama za matibabu, vikwazo vya nchi za Magharibi vya dawa na vifaa vya matibabu, pamoja na ukosefu wa usawa wa kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu kati baadhi ya maeneo nchini, ni miongoni mwa changamoto kubwa katika eneo hili. Katika baadhi ya vipindi, usimamizi mbaya, uhaba wa rasilimali na mashinikizo ya kiuchumi vimewafanya watu katika baadhi ya maeneo kutoridhishwa na huduma za afya. Ukweli huu hauwezi kupuuzwa. Lakini jambo muhimu ni kwamba, mfumo wa afya wa Iran, bado umesimama na unafanyiwa mageuzi na uboreshaji licha ya mashinikizo haya yote.

Mtazamo wa mustakabali, na ndani ya mfumo wa Hatua ya Pili ya Azimio la Mapinduzi, unafungua upeo mpya kwa uwanja wa afya na ustawi wa jamii. Kwa mtazamo huu, afya si matibabu ya magonjwa tu, bali pia inajumuisha afya ya kimwili, kiakili, kijamii na kiroho. Ustawi wa tiba za kuzuia magonjwa, mtindo wa maisha wenye afya, afya ya akili, msaada wa kifamilia, huduma bora zaidi kwa wazee na utumiaji wa teknolojia mpya kama vile utabibu wa kidijitali na akili mnemba katika utambuzi wa magonjwa na matibabu ni miongoni mwa mihimili ya baadaye katiika uwanja huu. Vilevile uadilifu wa kiafya, yaani kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za afya kati ya matabaka ya jamii na maeneo ya kijiografia, bado ni kipaumbele muhimu.

Mpenzi msikilizaji, kipindi hiki cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni fursa ya kuwashukuru na kuwaenzi madaktari, wauguzi, wafanyakazi na wahudumu wa afya ambao wamesimama mstari wa mbele katika kutoa huduma kwenye vipindi vigumu zaidi katika cha zaidi ya miongo minne iliyopita, kuanzia wakati wa vita vya kulazimiishwa hadi zama za janga la virusi vya corona. Badhi ya wahudumu hao wa afya wamepoteza maisha yao katika njia hiyo na majina yao yameandikwa baina ya mashahidi wa sekta ya afya. Huduma bora za afya za Iran ya leo ni matokeo ya kujitolea kwa watu hawa waliosabilia nafsi zao kwa ajili yetu. Hawa ni watu walioamini kwamba, kuwahudumia wanadamu ni ibada sawa kabisa na Swala na Swaumu.  *****