Jul 28, 2023 12:49 UTC
  • Hujjatul Islam Akbari: Walioivunjia heshima Qur'ani walitaka kuibua vita vya kidini

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria vitendo viovu vya kuchomwa moto Qur'ani Tukufu nchini Sweden na Denmark na kusema kuwa, waliokusudia kuibua vita baina ya wafuasi wa dini tofauti kwa kukivunjiwa heshima Kitabu hicho kitukufu wamefeli na kushindwa kufikia malengo yao.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari amesema hayo katika hotuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa Tehran na kubainisha kuwa, "Vitendo vya kuchukiza vilivyofanywa hivi karibuni dhidi ya Qur'ani Tukufu havijaambulia chochote." 

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Qur’ani Tukufu imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima na watu wenye misimamo mikali nchini Uswidi na Denmark, ambayo yalifanywa chini ya uangalizi wa serikali za nchi hizo.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari amesema, walioivunjia heshima Qurani Tukufu walikusudia kuibua migawanyiko baina ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo hasa Wakristo, lakini hawakufanikiwa kufikia malengo yao kwa kuwa Waislamu wanaheshimu Vitabu vitakatifu vya dini zingine.

Amesema moja ya malengo ya kuyavunjia heshima matukufu ya kidini ni kutaka kuwashughulisha walimwengu wasahau kadhia ya wananchi wa Palestina, lakini njama hizo zimefeli na kugonga mwamba.

Katika sehemu nyingine ya hotuba zake, Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema Imam Hussein (AS) aliarifisha hoja ya muqawama kwa waumini wote wa Kiislamu, na kwamba mapambano ndiyo njia pekee ya kupata mafanikio. Ameeleza bayana kuwa, hii leo harakati za muqawama wa Kiislamu katika pembe mbalimbai za dunia zimebaki hai kutokana na kujitoa muhanga Imam Hussein (AS).

Imam huyo wa muda wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amebainisha kuwa, Imam Hussein AS na Qurani Tukufu ni miangaza miwili kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo karibuni itaenea kote duniani.

Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya Iran wamehudhuria Swala hiyo ya Ijumaa iliyoswaliwa leo katika Chuo Kikuu cha Tehran, ikisadifiana na maadhimisho ya kumbukumbu ya Ashura ya Imam Hussein AS.

Tags