Tehran: Marekani itaachia fedha zinazoshikiliwa za Iran katika mchakato wa kubadilishana wafungwa
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kuhusiana na kuachiliwa rasilimali za Iran zinazoshikiliwa nje ya nchi, na vilevile kuachiwa huru idadi kadhaa ya wafungwa waliokuwa wakizuiliwa kinyume cha sheria nchini Marekani.
Ni baada ya baadhi ya vyanzo vya Iran kuthibitisha, jioni ya jana Alkhamisi, ripoti zilizochapishwa hapo awali kwamba Tehran na Washington zimekubali kubadilishana wafungwa.
Gazeti la New York Times hapo awali liliripoti kuwa wafungwa watano wa Kimarekani wataachiliwa huru kutoka gerezani mkabala wa kuachiliwa huru Wairani waliopatikana na hatia ya kukiuka vikwazo vya Marekani. Gazeti hilo pia lilidai kuwa takriban dola bilioni 6 za mauzo ya mafuta ya Iran zitaachiliwa.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema: Mchakato wa kuachiliwa mabilioni kadhaa ya dola, mali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yanayoshikiliwa kinyume cha sheria na Marekani kwa miaka kadhaa nchini Korea Kusini umeanza, na Iran imepata dhamana inayohitajika kwamba Marekani itatekeleza wajibu wake katika suala hili.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikifuatilia kwa makini suala la kuachiliwa rasilimali zake zinazoshikiliwa kinyume cha sheria na Marekani kwa visingizio visivyo na msingi, na vilevile kuachiwa huru raia wa Iran wanaoshikiliwa kinyume cha sheria nchini Marekani.
Taarifa hiyo imesema wafungwa wa Kimarekani bado wapo nchini Iran.