Amir-Abdollahian: Jitihada za kuhakikisha Iran inapata haki zake zote zinaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100988-amir_abdollahian_jitihada_za_kuhakikisha_iran_inapata_haki_zake_zote_zinaendelea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, sambamba na kuendelea jitihada za kufelisha vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi, juhudi za kidiplomasia ya kuhakikisha wananchi wa Iran wanapata haki zao zote, bado zinaendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 12, 2023 09:30 UTC
  • Amir-Abdollahian: Jitihada za kuhakikisha Iran inapata haki zake zote zinaendelea

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, sambamba na kuendelea jitihada za kufelisha vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi, juhudi za kidiplomasia ya kuhakikisha wananchi wa Iran wanapata haki zao zote, bado zinaendelea.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo Jumamosi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuandika kwamba, tangu ilipoingia madarakani seikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran imekuwa ikifanya jitihada za kupigiwa mfano za kidiplomasia kwa ajili ya kudhamini kiwango kikubwa zaidi cha manufaa ya taifa na kufanikisha kupatikana haki za taifa kubwa la Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, mchakato wa mazungumzo ya kidiplomasia unaendelea na hakuna wakati umewahi kusimama na kwamba juhudi zitaendelea hadi haki zote za Iran zitakapopatikana.

Alkhamisi usiku, tarehe 10 Agosti 2023, Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa tamko la kuthibitisha kuanza mchakato wa kuachiliwa mabilioni kadhaa ya fedha za Iran zilizokuwa zimezuiwa kidhulma na kinyume cha sheria na Marekani huko Korea Kusini na kusema katika taarifa yake hiyo kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mamlaka kamili ya jinsi ya kuzitumia fedha hizo ambazo hatimaye Marekani imelazimika kuziachilia huru katika makubaliano ya pande mbili ya kubadilishana wafungwa.