Maziko makubwa ya mashahidi wa shambulio la kigaidi la Shah Cheragh
Makumi ya maelfu ya Wairani wamewaaga wahanga wa shambulio la kigaidi la Jumapili kwenye Haram Takatifu ya Hadhrat Ahmad bin Musa (AS) maarufu kama Shah Cheragh mjini Shiraz kusini mwa Iran.
Katika hafla ya mazishi siku ya Jumatano, watu walibeba miili ya Gholm Abbas Abbasi, mhudumu wa haram takatifu, na Mohammad Jahnagiri, afisa wa usalama katika eneo hilo takatifu, kutoka Medani ya Mashahidi ya jiji hadi ua wa Haram ya Shah Cheragh.
Waombolezaji hao wamebeba mabango ya kulaani vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi yenye mafungamano na Daesh au ISIS na wafadhili wao wa nchi za Magharibi.
Huku wakipiga nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel," wameitaka serikali itoe jibu madhubuti na la kuleta majuto kwa wahalifu wote na wapangaji wa uhalifu huo mbaya.
Jumatano ilikuwa imetengwa kuwa siku ya maombolezo ya umma katika Mkoa wa Fars wa Iran. Siku ya Jumapili, gaidi kutoka Tajikistan aliendesha ufyatuaji risasi katika madhabahu ya Shah Cheragh, na kuua shahidi watu wawili na kujeruhi watu saba. Gaidi mmoja alikamatwa papo hapo na kukabidhiwa kwa vyombo vya sheria. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.
Ikumbukwe kuwa, mnamo Oktoba 26, 2022, gaidi mwenye silaha aliingia ndani ya eneo hilo la ibada, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama. Gaidi huyo baadaye alifariki hospitalini kutokana na majeraha aliyopata.