Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi la Shah Cheragh
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i101162-baraza_la_usalama_lalaani_shambulio_la_kigaidi_la_shah_cheragh
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa inayolaani shambulio la hivi karibuni la kigaidi katika Haram ya Shah Cheragh katika mji wa Shiraz.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2023 03:44 UTC
  • Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi la Shah Cheragh

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa inayolaani shambulio la hivi karibuni la kigaidi katika Haram ya Shah Cheragh katika mji wa Shiraz.

Katika taarifa yao hapo jana, nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zililaani shambulio hilo la kigaidi na la uoga dhidi ya watu wasio na hatia yoyote na mazuwari wa Haram ya Shah Cheragh.

Kadhalika nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimesisitiza kwamba, hatua ya kigaidii ya aina yoyote iile na inayofanyika kwa msukumo na malengo yoyote yale katu haikubaliki kwa namna yoyote ile. 

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo sambamba na kutoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi na familia za wahanga na mashahidi wa shambulio hilo imesisitiza juu ya udharura wa kuwajibika wale wanaowasaidia kifedha magaidi pamoja na waungaji mkkono wao.

Shambulio la kigaidi dhidi ya Haram ya Shah Cheragh 26/10/2022

 

Siku ya Jumapili, gaidi kutoka Tajikistan aliendesha ufyatuaji risasi katika haram ya Shah Cheragh, na kuua shahidi watu wawili na kujeruhi watu saba. Gaidi mmoja alikamatwa papo hapo na kukabidhiwa kwa vyombo vya sheria. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.

Ikumbukwe kuwa, mnamo Oktoba 26 mwaka jana (2022), gaidi mwenye silaha aliingia ndani ya eneo hilo la ibada, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama. Gaidi huyo baadaye alifariki dunia hospitalini kutokana na majeraha aliyopata.