Raisi na Modi wajadili njia za kuimarisha uhusiano wa Iran na India
Rais Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri Mkuu wa India Shri Narendra Modi wamejadili njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili, ushirikiano wa pande zote na utumizi wa uwezo kamili wa Bandari ya Chabahar.
Katika mazungumzo ya simu siku ya Ijumaa, Raisi alisema Iran na India zinapaswa hasa kupanua ushirikiano katika nyanja za usafiri na usalama wa nishati.
Rais wa Iran amesisitiza ushirikiano zaidi kwenye Ukanda wa Usafiri wa Kaskazini-Kusini.
Waziri Mkuu wa India kwa upande wake amelaani shambulizi la kigaidi dhidi ya Haram Takatifu ya Shah Cheragh katika mji wa Shiraz nchini Iran.
Modi amepongeza ushirikiano wa muda mrefu na Iran na kusema kutekelezwa mradi wa pamoja wa Bandari ya Chabahar ya Iran na kugeuzwa bandari hiyo kuwa kitovu cha uchukuzi kutapelekea maendeleo zaidi katika eneo.
Mohammad Jamshidi, mkuu wa maswala ya kisiasa katika Ofisi ya Rais wa Iran pia amechapisha ujumbe kwenye jukwaa la kijamii la X, ambalo zamani lilijulikana kama Twitter, kuhusiana na mazungumzo kati ya Raisi na Modi.
Afisa huyo ameandika kuwa: "Wamekubaliana kuharakisha kuendeleza Bandari ya Chabahar kama ishara ya ushirikiano wa pande mbili."
Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya India imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Raisi na Modi wamejadili masuala ya umuhimu wa nchi mbili na kikanda.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana mawazo kuhusu ushirikiano katika vikao vya kimataifa ikiwa ni pamoja na upanuzi wa kambi ya mataifa yanayoibukia kiuchumi ya BRICS kabla ya mkutano wake wa kilele mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 22-24.
Iran inatazamia kujiunga na BRICS, kundi lenye ushawishi mkubwa katika nchi zinazoendelea kiuchumi linalojumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.