Kanani: Marekani inapaswa kuondoka Syria kwa mujibu wa sheria za kimataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuhusu harakati za kijeshi za Marekani katika eneo hili kwamba kuwepo kijeshi nchi hiyo ya kibeberu katika ardhi ya Syria ni kinyume kabisa cha sheria.
Nasser Kanani, amesema hayo na kuongeza kuwa, serikali ya Syria haijawaalika wanajeshi wa Marekani kuingia nchini humo bali ombi rasmi la serikali ya Syria ni kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani nchini humo, haraka iwezekanavyo.
Matukio ya Syria yanaonesha kuwa, uwepo wa wanajeshi vamizi wa Marekani, mbali na kuwa ni kinyume cha sheria, lakini pia ndiyo sababu ya kuendelea kukosekana utulivu nchini humo. Mara kwa mara wakati magenge ya kigaidi yanapokaribia kusambaratishwa kabisa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya njama za kuyafanya magenge hayo yaendele kupumua. Amesema, hakuna sababu yoyote inayohalalilisha kuendelea wanajeshi wa Marekani kuweko nchini Syria, si sheria za kimataifa na wala si kwa mwaliko wa serikali ya Syria.
Suala la uingiliaji wa dola la kibeberu la Marekani katika masuala ya ndani ya nchi nyingine, limekuwa likilalamikiwa mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wiki iliyopita, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema kupanga na kufadhili mapinduzi, kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuwaunga mkono madikteta na magaidi ni katika sera kuu za Marekani na Uingereza katika kipindi chote cha historia.
Amma katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Kuna serikali rafiki katika ukanda huu kama vile Oman na Qatar, ambazo zina nia njema. Tunakaribisha juhudi zao nzuri katika kuhakikisha vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa letu vinaondolewa." Aidha amesema, Tehran haitopuuza kuchukua hatua yoyote ya kidiplomasia ya kufanikisha jambo hilo muhimu.