Iran yarejesha balozi wake Saudia; yasisitizia umuhimu wa ushirikiano wa kieneo
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kuna wajibu wa kuimarishwa ushirikiano wa pande zote wa nchi za eneo hili.
Rais Ebrahim Raisi amesema hayo wakati wa mazungumzo yake na balozi mpya wa Iran nchini Saudi Arabia na kusema kuwa, kustawi na kuongezeka ushirikiano wa nchi za ukanda huu kutaziinua nchi hizo katika milingano ya kimataifa.
Alireza Enayati, balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Saudi Arabia, alikutana na Rais Sayyid Ebrahim Raisi kwa ajili ya kupewa miongozo na nasaha za mwisho kabla ya kuelekea Riyadh kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu kama balozi kamili wa Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Rais Raisi amesisitiza kwenye mazungumzo hayo kwamba msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuendeleza na kuimarisha uhusiano na majirani zake, na amezitaja Iran na Saudi Arabia kuwa ni nchi mbili zenye taathira na ushawishi katika eneo hili na Ulimwengu mzima wa Kiislamu. Amesema, kuna haja ya kutumiwa vizuri nafasi na suhula zilizopo kuhakikisha uhusiano wa Tehran na Riyadh unaimarishwa kadiri inavyowezekana.
Vilevile amesema: Ushirikiano wa Iran na Saudi Arabia na kuongezeka ushirikiano wa nchi za eneo eneo hili katika nyuga tofauti za baina ya pande mbili na pande kadhaa na katika masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu kiujumla; katika ngazi za serikali na wananchi wa kawaida, kutaimarisha nafasi ya nchi za eneo hili kwenye milingano ya kikanda na kimataifa na kuzuia uingiliaji wa madola ajnabi katika masuala ya nchi hizo.