Dola bilioni 1.7 za Iran zilizokuwa zimezuiliwa Luxemburg zaachiwa
(last modified Sun, 08 Oct 2023 03:24:31 GMT )
Oct 08, 2023 03:24 UTC
  • Dola bilioni 1.7 za Iran zilizokuwa zimezuiliwa Luxemburg zaachiwa

Dola bilioni 1.7 katika hazina ya fedha za kigeni za Iran zilizokuwa zimezuliwa nchini Luxemburg zimeachiliwa.

Kwa mujibu wa ISNA, kufuatia hatua na ufuatiliaji wa kisheria uliofanywa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Luxemburg, vizuizi vya kimahakama vilivyokuwa zimewekewa milki za fedha za kigeni za Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo kiwango chake ni dola bilioni moja na milioni 700 zilizokuweko nchini Luxemburg vimeondolewa, na kuanzia sasa hivi fedha hizo zinaweza kutumiwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa mali na milki za fedha za kigeni za benki hiyo zilizokuwa zimezuiliwa na Taasisi ya Clearstream ya nchini Luxembourg mwaka 2020 kutokana na mashtaka yaliyowasilishwa na baadhi ya raia wa Marekani, hatimaye zimeachiliwa baada ya malalamiko na ufuatiliaji wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, uliopelekea Mahakama ya Juu ya Luxembourg kutoa uamuzi mnamo Septemba 28, 2022 wa kukubali hoja zilizowasilishwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 
Kabla ya hapo, Davood Manzoor, Mkuu wa Shirika la Mipango na Bajeti la Iran alitangaza kuachiliwa kwa fedha za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilizokuwa zimezuiliwa katika nchi za Japan, Uturuki, Korea Kusini na Iraq.
 
Kupitia mpango wake wa uwekaji vikwazo na sera yake ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran, Marekani ilikuwa imezizuia kinyume cha sheria baadhi ya rasilimali za fedha na mali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.../