May 27, 2024 10:27 UTC
  • Kuendelea uthabiti wa sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Baada ya kufa shahidi Seyyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Hossein Amir Abdullahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya 13, suala la kudumishwa uthabiti wa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepewa mazingatio makubwa.

Sera ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kiislamu imejikita katika kupinga ubeberu na uistikbari duniani. Katika ibara  pili, kipengele cha tano cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kunapinga kila aina ya dhulma na ukandamizaji. Aidha katika ibara ya tatu, kipengele cha tano Katiba ya Iran inapinga vikali ukoloni, ushawishi na upenyezaji wa nchi ajinabi katika masuala ya nchi. "Heshima, hekima na maslahi" ni misingi mitatu mikuu na ya kudumu katika sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja misingi hiyo kuwa "pembetatu" ya lazima kwa mfumo wa Kiislamu katika uhusiano wake wa kimataifa" na pia kubainisha kuhusu maingiliano ya Iran na mataifa ya kigeni katika ruwaza ya miaka ishirini ya nchi kwa kuzingatia misingi hiyo mitatu.

Wakati huo huo, kukabiliana na ukiritimba wa madola ya Magharibi katika mahusiano ya kigeni imekuwa moja ya siasa muhimu za serikali ya 13. Nukta hii ilipewa umuhimu hasa kwa kuzingatia kwamba muhimili wa nguvu katika mfumo wa ulimwengu sasa unahama kutoka Magharibi kuelekea Mashariki. Kuhusiana na hilo, kuingia katika uhusiano wa kistratijia na madola ya mashariki hususan Russia na China kumezingatiwa kikamilifu na serikali ya awamu ya 13 ya Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi ili kukabiliana na ubeberu wa nchi za Magharibi. Serikali ya 13 imeonyesha kuwa inaamini kuhusu mlingano katika sera za kigeni hasa kuhusu ushirikiano na majirani, nchi za Kiislamu na za Afrika.

Nukta muhimu ni kwamba sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu zinatekelezwa ndani ya mfumo wa kitaasisi na hivyo hazitegemei watu binafsi katika utekelezaji wake.

Mashahidi Rais Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Amir Abdollahian wakiwa safarini nchini Kenya

Kwa msingi huo, hata baada ya kufa shahidi Rais na Waziri wa Mambo ya Nje, sera za kigeni za Iran zitaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia misingi na kanuni zilizoainishwa kuhusu maendeleo ya siasa za ujirani mwema na upanuzi wa uhusiano na nchi za dunia katika mabara tofauti.

Bila shaka, hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika siasa za kimsingi za Iran katika kutoutambua utawala haramu wa Israel, jambo ambalo limesisitizwa tangu kuundwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati huo huo, serikali yoyote ijayo ya Iran itaendeleza upanuzi wa uhusiano na nchi jirani na suala hilo litapewa kipaumbele. Baada ya hapo sera za kigeni zinatilia mkazo kuimarishwa uhusiano na nchi nyingine katika mabara tofauti ya dunia.

Aidha, Iran itaendelea kuwa na uwepo hai na wenye nguvu katika mashirika ya kieneo kama vile Shirika la Ushirikiano la Shanghai, BRICS na mashirika mengine ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na taasisi zake tanzu.

 

Tags