Muda wa vikwazo kwa makombora ya balestiki ya Iran umemalizika
(last modified Thu, 19 Oct 2023 02:26:10 GMT )
Oct 19, 2023 02:26 UTC
  • Muda wa vikwazo kwa makombora ya balestiki ya Iran umemalizika

Vikwazo kwa mradi wa makombora ya balestiki ya Iran vilivyokuwa vimewekwa na Umoja wa Ulaya vilifikia kikomo Jumatano ya jana Oktoba 18, chini ya Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliidhinisha mkataba wa nyuklia wa JCPOA wa mwaka 2015.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Ali Baqeri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: Iran haikabiliwi tena na vizingiti vya aina yoyote juu ya shughuli za makombora yake ya balestiki katika fremu ya Baraza la Usalama la UN.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, kuwekewa vikwazo vipya Jamhuri ya Kiislamu ni ukiukaji wa wazi wa matini ya Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Mkataba wa nyuklia unaojulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ulisainiwa mwezi Julai 2015 kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambazo ni Marekani, Russia, China, Uingereza na Ufaransa pamoja na Ujerumani.

Ali Baqeri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa

Aidha tovuti ya Umoja wa Mataifa ulichapisha jana Jumtano taarifa kuhusu na kumalizika muda wa vikwazo hivyo dhidi ya mradi wa makombora ya balestiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

UN imechapisha orodha ya mali na taasisi za Iran zilizokuwa zimewekewa vikwazo kutokana na mradio huo wa makombora na kueleza bayana kuwa, orodha hiyo imeondolewa rasmi kutoka kwenye tovuti ya umoja huo.

Majeshi ya Iran yamekuwa yakisisitiza kuwa, utumiaji wa makombora ya balestiki ambayo yana uwezo ya kulenga shabaha zilizokusudiwa ni mafanikio makubwa ya kiulinzi kwa Jamhuri ya Kiislamu.