Abdollahian na Haniya wakutana Doha na kujadili matukio ya Ukanda wa Gaza
(last modified Wed, 01 Nov 2023 04:34:53 GMT )
Nov 01, 2023 04:34 UTC
  • Abdollahian na Haniya wakutana Doha na kujadili matukio ya Ukanda wa Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdollahian na Ismail Haniya walikutana na kufanya mazunugumzo hayo jana Jumanne huko Doha, mji  mkuu wa Qatar.

Huu ni mkutano wa pili baina ya wawili hao, tangu baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kupata ushindi katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyoanza Oktoba 7.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Hakuna shaka taifa na kambi ya muqawama wa Palestina wataibuka washindi katika makabiliano na utawala wa Kizayuni. 

Amebainisha kuwa, "Utawala wa Kizayuni umeporomoka, na hakuna shaka kuwa matokeo ya makabiliano haya ni ushindi wa kishindo kwa wananchi na muqawama wa Palestina."

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameitaja hali ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza kuwa ni ya kusikitisha kutokana na mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na matokeo yasiyotabirika ya jinai hizo.

Wawili hao wamezungumzia pia udharura wa kusitishwa haraka iwezekanavyo mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na kutumwa misaada endelevu na mikubwa ya kibinadamu kwa ajili ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. 

Tags