Abdollahian: Unyama wa utawala wa Israel huko Gaza una utambulisho wa Kidaesh
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: Mienendo isiyo ya kibinadamu ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia mateka wa Palestina katika ukanda wa Gaza ni mfano na ishara ya wazi ya tabia ya kundi la kigaidi la Daesh.
Hossein Amir- Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hayo mjini Geneva Uswisi katika kikao cha ngazi ya juu cha Mawaziri kuhusu "Hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Haki za Binadamu za Kimataifa" kilichohudhuriwa na idadi kubwa ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi mbalimbali wakiwemo wa baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu na wanadiplomasia waandamizi ambapo alifafanua na kueleza mitazamo ya Iran kuhusu hali ya mgogoro wa Palestina na hali ya kutisha ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutokana na kuendelea mashambulizi ya kijinai ya utawala wa Kiizayuni wa Israel.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amezihesabu hatua za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina katika ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kuwa ni mifano ya wazi isiyo na shaka ya jinai za kivita na mauaji ya kimbari.
Amir Abdollahian aidha ametangaza wajibu wa haraka wa jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua madhubuti za kusimamisha mara moja mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kukomesha jinai za utawala huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kutuma misaada ya kibinadamu.
Ameitaja mienendo isiyo ya kibinadamu ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia mateka wa Palestina katika ukanda wa Gaza kuwa ni mfano na ishara ya tabia za kidaeshi za utawala huo ghasibu wa Israel.