Meja Jenerali Salami: Hakuna nchi yenye ujasiri wa kuishambulia Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Hivi sasa hakuna nchi yenye ujasiri wa kushambulia taifa na ardhi ya Iran.
Meja Jenerali Hossein Salami, Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema jana Alkhamisi katika kumbukumbu ya mashahidi 10,000 wa mkoa wa Azarbaijan Mashariki (Kaskazini Magharibi mwa Iran), kuwa nguvu ya Iran ya Kiislamu ni urithi wa kudumu wa mashahidi na kuongeza kuwa: "Mashahidi waliifikisha Iran kwenye kilele cha heshima na katika zama hizi, wanasiasa na watu binafsi wa maeneo mbalimbali ya dunia wanaizungumzia Iran kwa heshima na taadhima."
Akiashiria kwamba maadui bado wanafanya mikakati ya kuyanyima mataifa ya Kiislamu haki zao, Meja Jenerali Salami amesema: Wanataka kukalia kwa mabavu ardhi zaidi za Waislamu kama vile Palestina na mfano wa wazi ni mashambulio yanayoendelea kufanyika huko Gaza.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelaani hujuma zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika hospitali, makazi ya raia na vituo vya huduma mbalimbali na kusema mauaji ya watoto wachanga ndio fahari ya utawala wa Kizayuni, na Wazayuni wanakuona kuuawa shahidi raia, watoto, wazee na wanawake kuwa ndio ushindi.
Meja Jenerali Salami ameeleza kuwa, hivi sasa chuki ya umma dhidi ya utawala wa Kizayuni imefika kileleni baina ya mataifa ya dunia na kusema: Mataifa yote yamejitosa uwanjani kuiunga mkono Palestina na kutangaza kuchukizwa kwao na uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, idadi ya mashahidi waliouawa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba imefikia 18,608.