Seneti ya Kenya yapinga pendekezo la kuongezwa muhula wa Rais
Kamati ya Seneti ya Kenya kuhusu Haki na Masuala ya Sheria inayoongozwa na Seneta wa Bomet, Hillary Sigei, imeitaka Seneti isipitishe muswada unaopendekeza kuongezwa muhula wa Rais na viongozi waliochaguliwa.
Muswada wa Marekebisho ya Katiba uliowasilishwa na Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, unapendekeza muhula wa kuhudumu wa rais, maseneta, magavana na wabunge kuongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.
Kamati hiyo imesema kwamba Wakenya wengi wamepinga pendekezo hilo.
“Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Sheria na Haki za Kibinadamu inapendekeza kuwa Seneti isipitishe Muswada wa Marekebisho kuhusu Katiba ya Kenya nambari 2, 2024, Miswada ya Seneti, Nambari 46 ya 2024,” imesema ripoti hiyo.
Kamati hiyo pia imeagiza Kamati ya Seneti kuhusu Taratibu na Sheria iangazie upya mchakato unaoruhusu kujadiliwa kwa pendekezo la kisheria kuhusu kufanya marekebisho ya Katiba ikiwemo kuanzisha marekebisho ya kanuni za seneti.
Pendekezo kama hilo litahitaji kuwa na saini ya angalau maseneta 15 wanaoliunga mkono, isipokuwa tu linapowasilishwa na Walio Wengi au Walio Wachache.
Katika ripoti yake, kamati imesema imepokea barua pepe kutoka kwa maelfu ya Wakenya wakipinga vikali pendekezo la kuongeza muda wa hatamu za urais na viongozi waliochaguliwa.
Ripoti ya kamati hiyo imesema: “Asilimia 99.99 ya maoni yaliyopokewa yamepinga vikali muswada huo kwa jumla au vipengele vilivyohusu kuongezwa muda wa kuhudumu wa rais, wabunge, magavana, na madiwani kutoka miaka mitano hadi saba.”