Kuendelea hatua na misimamo ya undumakuwili ya Marekani dhidi ya Iran
(last modified Sat, 02 Nov 2024 11:15:28 GMT )
Nov 02, 2024 11:15 UTC
  • Kuendelea hatua na misimamo ya undumakuwili ya Marekani dhidi ya Iran

Rais Joe Biden wa Marekani jana Ijumaa aliwatumia barua wakuu wa bunge la wawakilishi na seneti ambapo amerefusha kwa mwaka mmoja mwingine muda wa hali ya hatari kitaifa kuhusu Iran. Biden amechukua hatua hii katika miezi yake ya mwisho akiwa White House na kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais wa Marekani tarehe 5 mwezi huu wa Novemba.

Biden amesema katika barua hiyo kuwa: "Hali ya hatari kitaifa kuhusu Iran ambayo ilitangazwa katika Dikrii ya Utekelezaji nambari 12170 mnamo Novemba 14 mwaka 1979 itaendelea baada ya Novemba14 mwaka huu." Rais Biden ameongeza kuwa: "Uhusiano wetu na Iran bado si wa kawaida, na mchakato wa utekelezaji wa makubaliano tuliyofikia kuhusu Iran  Januari 19 mwaka 1981 bado unaendelea. Hivyo, nimeona kuna udharura wa kuendelea hali ya hatari ya kitaifa iliyotangazwa katika Agizo la Utekelezaji nambari 12170 kuhusiana na Iran." 

Jimmy Carter Rais wa zamani wa wakati huo wa Marekani mnamo Novemba 14 mwaka 1979 aliagiza kutekelezwa Dikrii ya Utekelezaji nambari 12170, siku 10 baada ya kutekwa ubalozi wa Washington mjini Tehran; ambapo alitaka kuzuiwa mali za serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Marekani na  kuanzia mwaka huo hadi leo marais wote wa Marekani wamekuwa wakirefusha muda huo.

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter 

Hatua ya Biden ya kuongeza muda wa hali ya hatari ya kitaifa dhidi ya Iran inaonyesha kuendelea makabiliano halisi ya Marekani dhidi ya Iran yaani muendelezo wa hatua za uhasama na uadui dhidi ya wananchi wa Iran. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran; Marekani ambayo ilikuwa kinara wa kambi ya Magharibi huku ikifanya kila linalowezekana ili kuwa na ushawishi katika eneo la Asia Magharibi ilidhihirisha uhasama na uadui dhidi ya Iran na kulifanya suala la kuipindua madarakani Jamhuri ya Kislamu ya Iran kuwa kipaumbele cha sera zake. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Marekani imekuwa ikitekeleza sera na hatua nyingi za upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa njia mbalimbali, kama vile kuiwekea nchi hii vikwazo vikubwa zaidi, kuitishia kijeshi, kuanzisha kampeni za kisiasa na kidiplomasia na vita vya kisaikolojia. 

Licha ya kufeli na kugonga mwamba sera na hatua za upande mmoja za Marekani dhidi ya Iran, lakini Washington ingali inang'ang'ania kuendelezwa hatua hizo zisizo za kisheria na zinazokinzana na Hati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Tehran; ambapo katika duru ya uongozi wa Rais Joe Biden, Marekani imeshadidisha vita mchanganyiko dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa visingizio mbalimbali. Tangu aingie madarakani Januari 2021 na licha ya nara na ahadi zake za awali, Biden ameendeleza kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu, na mara kadhaa ametangaza kuiwekea Iran vikwazo vipya kwa visingizio mbalimbali.  

Kwa kuzingatia kuwa mwaka huu Marekani inaendesha uchaguzi wa Rais na uchaguzi wa katikati ya muhula wa Kongresi ya nchi hiyo, Donald Trump mgombea wa chama cha Republican katika kampeni zake za uchaguzi anajaribu kuvutia hisia za lobi na duru za Kizayuni nchini Marekani kama vile lobi ya AIPAC kwa kutoa kauli na matamshi dhidi ya Iran. Bila shaka Joe Biden na sasa Kamala Harris mgombea wa chama cha Democrat licha ya kuendelea na kushadidi vikwazo dhidi ya Iran wamesema: Machaguo yote mkabala wa Iran yako mezani huku wakikariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya nchi hii. 

Suala muhimu ni kuwa, undumakuwili wa wazi unashuhudiwa katika siasa za Marekani dhidi ya Iran. Moja ya tuhuma za mara kwa mara za Washington dhidi ya Tehran ni eti kwamba Iran inafanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia; na kwa kisingizio hicho, Marekani imeiwekea Iran vikwazo vikali ambavyo havijawahi kushuhudiwa tangu wakati wa utawala wa Rais George Bush. Hata hivyo, msingi wa tuhuma hizi umetiliwa shaka si tu katika ripoti nyingi za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) bali pia na idara za ujasusi za Marekani. 

Wakala wa IAEA umethibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Iran ni ya malengo ya amani 

Sehemu ya ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Intelijensia ya Marekani mwezi Julai 2023, ilisisitiza kuwa Iran kwa sasa haitekelezi shughuli zinazohitajika kutengeneza bomu la nyuklia hata hivyo inaendelea na shughuli zake za utafiti na maendeleo yenye malengo ya amani. 

Iran imetoa jibu thabiti na la wazi kwa vitisho vya Marekani dhidi yake ambavyo vimetolewa kupitai matamshi ya mara kwa mara ya marais wa nchi hiyo wanaodai kuwa machaguo yote  dhidi ya Iran yako mezani. Hili linaonyesha kuwa, Tehran, huku ikiimarisha uwezo na nguvu zake za kuzuia na kutoa jibu kali kwa hujuma ya adui dhidi yake, si tu kuwa haihofii vitisho vya Washington, bali itatoa jibu kali na madhubuti iwapo kutajiri chokochoko zozote za Marekani dhidi yake.  Aidha, kurefushwa muda wa hali ya hatari dhidi ya Iran, hatua ambayo Biden pia ameitekeleza hakuyumbishi kivyovyote vile azma ya Tehran ya kukabiliana na njama za Washington.