Israel yaililia Russia iwe mpatanishi kati yake na Hizbullah
(last modified Sat, 02 Nov 2024 11:14:47 GMT )
Nov 02, 2024 11:14 UTC
  • Israel yaililia Russia iwe mpatanishi kati yake na Hizbullah

Israel sasa inaiasa Russia eti ishiriki katika 'juhudi za amani' zinazolenga kumaliza mzozo kati ya utawala huo wa Kizayuni na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Vyombo vya habari vya Kizayuni huku vikiwanukuu maafisa wa Israel wanaohusika na mazungumzo hayo vimeripoti kuwa, Tel Aviv inataraji kuwa, ushiriki wa Moscow kwenye mazungumzo hayo mbali na kuimarisha uthabiti katika makubaliano tarajiwa, lakini pia utapunguza utegemezi wa Marekani.

Shirika la habari la Russia Today limenukuu ripoti ya vyombo vya habari vya Kizayuni vikisema kuwa, "Warusi watakuwa na jukumu maalumu katika kutekelezwa makubaliano na kuzuia kuongezeka mvutano." 

Akizungumzia ripoti hizo, Orna Mizrahi, afisa wa zamani wa Israel katika mahojiano na Newsweek amedai kwamba, ingawaje Israel "inawafadhilisha Wamarekani," lakini inaelewa kwamba "uhusiano mzuri" wa Russia na Iran unaweza kuchangia kufikiwa makubaliano madhubuti na Lebanon.

Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zilidai wiki hii kwamba, mazungumzo kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon tayari yamefikia "hatua za juu."

Wazayuni wanaendelea kukabiliwa na vipigo kutoka kwa wanamuqawama wa Hizbullah

Mjumbe wa Rais wa Marekani Joe Biden, Amos Hochstein, ambaye ni mpatanishi kati ya Israel na Lebanon, aliripotiwa kufikia makubaliano ya awali juu ya mpango huo wakati wa safari ya Beirut mapema wiki hii.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kukumbwa na kiwewe kutokana na vipigo vikali vya makombora na droni unavyoendelea kupokea kutoka kwa wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon.