Iran: Tuna uwezo wa kupiga nukta yoyote ya Israel wakati wowote tunapopenda
Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Iran ina uwezo mkubwa wa kiulinzi kiasi kwamba leo hii inaweza kupiga nukta yoyote ya Israel kwa makombora yanayopiga vizuri mno shabaha, wakati wowote itakapoona kuna haja ya kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Hujjatul Islam Mohammad Mohammadi Golpayegani alisema hayo jana mjini Qom, kusini mwa Tehran na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vina uwezo mkubwa kiasi kwamba hata madola makubwa yenye nguvu za nyuklia dunia kama Russia na China zinaomba msaada wa Iran.
Aidha amesisitiza kwa kusema, kadhia ya Ghaza ni ya Wapalestina lakini Wapalestina wameifanya Iran kuwa ndicho kigezo chao na kwamba makundi ya mapambano na muqawama wa Kiislamu ya Palestina na kusimama kwao imara mbele ya jinai za kutisha za utawala ghasibu wa Kizayuni yote yanaifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa ndicho kigezo chao.
Ameongeza kuwa, leo hii Wayemen wamekuwa na nguvu kiasi kwamba wamezilazimisha meli za utawala wa Kizayuni zishindwe kupita kwenye Bahari ya Sham na zizunguke masafa marefu hadi kufika zinakokwenda, suala ambalo linausababishia hasara ya mabilioni ya dola utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amelaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni za kuua vitoto vichanga na wananchi wa kawaida wasio na hatia huko Palestina hasa Ghaza na kusema kuwa, serikali ya Marekani na hususan rais mwenyewe wa dola hilo la kiistikbari, Joe Biden, wanashiriki moja kwa moja kwenye jinai hizo za Wazayuni.
Ameongeza kuwa vita vya Ghaza vimewafedhehesha Wazayuni na madola ya kibeberu na sasa walimwengu wamezidi kugundua uongo wa Wazayuni na madola ya kibeberu katika madai yao mbalimbali.