Jenerali Salami: Kinachojiri Gaza ni mauaji ya halaiki
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) sanjari na kulaani jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza amesisitiza kuwa, "Kinachojiri Gaza ni mauaji ya halaiki."
Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH akisema hayo na kuongeza kuwa, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanapasa kuwatanabahisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja
Meja Jenerali Salami ameyataka mataifa ya Kiislamu kuwa na umoja na mshikamano ili kuvunja njama na jinai za Wazayuni na washirika wake dhidi ya Wapalestina.
Kamanda Mkuu wa SEPAH ameashiria umuhimu wa mataifa ya Kiislamu kukumbatia sekta ya sayansi na teknolojia na kueleza kuwa: Iran yenye nguvu ina nafasi muhimu katika kuujenga ustaarabu imara duniani.
Kamanda Salami amewataka vijana wa Kiislamu kuikoa sekta ya sayansi kutokana kwenye ukiritimba wa madola maovu, na wafanye jitihada za kujiimarisha na kuboresha jamii zao kupitia sayansi.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: Kwa mujibu mantiki ya madola ya kishetani ya dunia ya leo, mataifa dhaifu hayana nafasi yoyote katika ramani ya siasa za dunia.
Ameonegeza kuwa, matukio ya Gaza ni aina fulani ya mauaji ya umati na kuonya kwamba, matawi ya sayansi yapo katika mikono ya maadui wenye nia ya kuisambaratisha dunia ili wawe na nguvu zaidi.