Kujiunga rasmi Iran na kundi na BRICS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106714-kujiunga_rasmi_iran_na_kundi_na_brics
Mwakilishi wa Afrika Kusini katika Kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani (BRICS) ameeleza kuwa Iran, Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ethiopia zimejiunga rasmi na kundi hilo kuanzia Januari Mosi mwaka huu wa 2024.
(last modified 2024-01-02T04:36:51+00:00 )
Jan 02, 2024 04:36 UTC
  • Kujiunga rasmi Iran na kundi na BRICS

Mwakilishi wa Afrika Kusini katika Kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani (BRICS) ameeleza kuwa Iran, Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ethiopia zimejiunga rasmi na kundi hilo kuanzia Januari Mosi mwaka huu wa 2024.

Anil Sooklal ameashiria kushiriki wawakilishi wa ngazi ya juu wa Iran, Saudi Arabia, Misri na Ethiopia katika kikao cha karibuni cha kundi la BRICS kilichofanyika Disemba Mosi mwaka jana huko Durban nchini Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, nchi wanachama wa BRICS zitaongezeka mara mbili kufuatia kujiunga nchi hizo. 

Wawakilishi wa nchi mpya wanachama wa BRICS wanatazamiwa kushiriki katika mkutano ujao wa kiuchumi wa kundi hilo uliopangwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu huko Moscow, mji mkuu wa Russia. 

Nchi waasisi wa BRICS ambazo ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka jana zilizialika nchi 5 mpya ambazo awali ziliwasilisha maombi yao ya kupatiwa uanachama kujiunga na kundi hilo la kiuchumi, na kwa utaratibu huo, baadhi ya  wazalishaji wakubwa wa nishati duniani wanakutana pamoja na baadhi ya watumiaji wakubwa wa nishati duniani katika kalibu ya kundi la  BRICS. 

Wanachama waasisi wa BRICS

Kama alivyosema Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia: Hivi sasa karibu nchi 30 duniani zinataka kuwa wanachama wa kundi la BRICS.  

Kustawisha uhusiano na kupanuliwa ushirikiano wa pande kadhaa kimataifa katika kalibu ya jumuiya na taasisi kama ile ya Shanghai, BRICS au Euroasia ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran inayoongozwa na Rais Sayyid Ebrahim Raisi; hatua ambazo zinatekelezwa kwa lengo la kukuza uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na pia kama njia ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani. 

Moja ya sababu kuu zinazolifanya kundi la BRICS kuwa na umuhimu ni uwezo wake mkubwa ni kukua kwa kasi uchumi na ushawishi wa kundi hilo katika masuala ya kimataifa; ambavyo  ni maokeo ya kuwa na nusu ya jamii ya watu duniani, asilimia baina 25 na 28 ya uchumi wa dunia na vilevile rasilimali watu na maliasili tajiri.

Mwenendo wa  matukio ya kiuchumi na kiviwanda ya wanachama wa BRICS unaonyesha  kuwa msingi wa harakati na fikra ya kuasisiwa kundi hilo kuwa na nafasi na mchango mkubwa katika ulimwengu wa kambi kadhaa na kutoa ushindani na changamoto kwa mfumo unaotawala sasa duniani.   

Kila nchi mwanachama wa kundi la BRICS inahesabiwa kuwa na nafasi na mchango muhimu masuala ya kisiasa au kiuchumi ya eneo na kanda yake. Wakati huo huo nafasi ya kipekee ya kijiografia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uwezo wake katika nyanja za nishati, usafirishaji na biashara inaweza kuwa ya manufaa kwa nchi nyingine wanachama BRICS.

Miongoni mwa mambo ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepanga kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wanachama wengine wa kundi hilo ni suala la kuacha kutumia sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara na kiuchumi na kushirikiana katika masuala ya fedha.  

Hivi sasa suala la kuachana na matumizi ya sarafu ya dola duniani khususan kwa nchi zilizo chini ya vikwazo kama Iran na Russia, linazingatiwa pakubwa na nchi kadhaa duniani; ambapo kwa hakika hatua ya Marekani ya kutumia sarafu ya dola kuzishinikiza nchi huru duniani katika miongo kadhaa iliyopita ni kati ya sababu kuu zilizotoa msukumo na kuzifanya nchi mbalimbali kutafuta njia mbadala wa kufanya miamala ya kifedha na kibiashara bila ya kutegemea sarafu ya dola. 

Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Paul Mashatile, amesema kuhusiana na suala hili kuwa, wanachama wa BRICS wanalenga zaidi kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola ya Marekani; leo hii dunia inalipa umuhimu kundi la BRICS kwa sababu liko mstari wa mbele katika mazungumzo ya kimataifa ya kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola. 

Suala jingine lenye  maslahi kwa BRICS ni uundaji wa kile kinachojulikana kama  "international currency reserve" kwa kuzingatia sarafu ya nchi wanachama. BRICS pia inajaribu kukabiliana na taasisi za fedha za Magharibi kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa kuasisi benki mpya ya maendeleo na hifadhi ya sarafu ya pamoja.