Kiongozi Muadhamu: Mkakati mkuu wa Iran ni kutegemea nguvu laini
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mkakati mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi hiki cha miaka 45 iliyopita ni kutegemea nguvu laini na nguvu hizo zinapaswa zifanywe kubwa zaidi.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano wakati alipoonana na maelfu ya wasomaji kasida na mashairi ya Ahlul Bayt AS. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra SA amesisitiza kuwa, kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Khomeini (MA) ambaye ni mbeba bendera ya Jihadi ya Bibi Fatima SA kunakumbushia jitihada na jihadi kubwa za Luteni Jenerali Qassem Soleimani (aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH).
Amesema, Bibi Fatimatuz Zahra aliweka jiwe la msingi la Jihadi ya kubainisha ukweli na kusisitiza kuwa, wasomaji wa kasida na mashairi ya Ahlul Bayt AS wanapaswa kuendelea kuifanya kigezo chao bora jihadi hiyo na somo kubwa linalopatikana ndani yake.
Ameongeza kuwa, Jihadi ya kubainisha ukweli na uhalisi wa mambo mbali na nguvu zake za kutikisa nyoyo na kuleta harakati za kimapinduzi, iko makini pia katika kuainisha malengo muhimu zaidi kwani baadhi ya wakati katika sehemu ambayo panahitajika mno umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu kunafanyika uzembe na kuishia kwenye kuzuka mizozo na migogoro katika safu za Waislamu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, vile vile amesema, miongoni mwa athari za nguvu hizo laini za Iran ni kukimbia kwa madhila Marekani huko Afghanistan na kuchukiwa mno dola hilo la kibeberu na wananchi wa Iraq.
Amma kuhusu Palestina na vita vinavyoendelea huko Ghaza, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, wananchi wa Ghaza leo hii hawapambani na utawala wa Kizayuni tu bali wanapambana na dunia yote ya ukafiri, utaghuti na uistikbrai hasa kutokana na kuwa, rais wa Marekani ametangaza waziwazi kwamba yeye ni Mzayuni akiwa ni maana kwamba ule ukhabithi wote mchafu walio nao Wazayuni, na yeye pia anao.