Ugaidi, njama iliyoshindwa ya maadui dhidi ya Iran ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106810-ugaidi_njama_iliyoshindwa_ya_maadui_dhidi_ya_iran_ya_kiislamu
Maadui wa Iran ya Kiislamu kwa mara nyingine tena wamewaua shahidi na kuwajeruhi mamia ya raia katika kitendo cha kigaidi.
(last modified 2024-01-04T08:31:06+00:00 )
Jan 04, 2024 08:31 UTC
  • Ugaidi, njama iliyoshindwa ya maadui dhidi ya Iran ya Kiislamu

Maadui wa Iran ya Kiislamu kwa mara nyingine tena wamewaua shahidi na kuwajeruhi mamia ya raia katika kitendo cha kigaidi.

Jumatano alasiri, milipuko miwili ya kigaidi ilitokea katikati mwa umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakishiriki marasimu ya kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu,  katika barabara inayoelekea kwenye makaburi ya mashahidi huko Kerman, ambayo ilipelekea kuuawa shahidi watu 103 na kujeruhiwa wengine 284.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza baada ya kuuawa shahidi kundi kubwa la watu kwenye kaburi la Shahidi Soleimani kwamba: Wahalifu  wanajua kwamba askari wa njia ya Soleimani hawatastahamili jinai zao.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku akilaani jinai hiyo ya kigaidi huko Kerman, ameitaja kuwa ni ya maadaui wa Iran na pamoja na kutaka kushughulikiwa haraka majeruhi wa tukio hilo amesistiza haja ya kufuatiliwa na kukamatwa wahusika na kitendo hizo kichafu na cha uoga.

Eneo la tukio

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ugaidi duniani, na hadi sasa zaidi ya watu na maafisa wake 17,000 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi. Kwa hakika tokea mwanzoni mwa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuvurugwa mfumo wa kistakibari duniani, Iran imekuwa mlengwa mkuu wa chuki na uadui wa maadui, hasa Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wake. 

Kutoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi, misaada ya kifedha, habari za kiusalama na kuwapa silaha na vifaa vya mawasiliano ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na maadui katika kuimarisha makundi ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani mnamo Januari 13, 2018, shambulio dhidi ya makao ya polisi huko Rask katika mkoa wa Sistan na Baluchistan mwezi Desemba uliopita, shambulio la kigaidi kwenye Haram ya Imam Ridha (as) mapema mwaka uliopita, shambulio la magaidi wa Daesh katika Haram ya Imam Khomeini (RA)  na Majlis ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) mnamo mwaka 2018, mlipuko katika Haram ya Imam Ridha (as) mwaka 1997 na mauaji ya wanasayansi kama Mohsen Fakhrizadeh mwaka 2021 ni miongoni mwa mashambulio ya kigaidi ambayo yametekelezwa na maadui na vibaraka wao nchini Iran.

Majeruhi wa tukio hilo la kigaidi

Kuchochea ghasia na kuvuruga mfumo wa usalama wa taifa, kuwatia hofu na wasiwasi wananchi na kuwafanya raia wazingatie zaidi masuala ya kimaada ili kuzuia kufikiwa malengo muhimu Mapinduzi ya Kiislamu, ni miongoni mwa mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa na maadui na washirika wao katika uwanja huo.

Pamoja na vitendo vyote hivyo vya kigaidi dhidi ya wananchi na viongozi wa Iran lakini hadi sasa, jumuiya za kimataifa si tu kwamba hazijachukua hatua yoyote muhimu na ya kivitendo kwa ajili ya kuzuia kukaririwa jinai hizo, bali serikali zinazounga mkono na kuwafadhili magaidi hao daima zimekuwa zikikanusha kuhusika na vitendo hivyo. Kwa mfano, Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, amedai kuhusu tukio la kigaidi katika eneo la makaburi ya mashahidi wa  Kerman kwamba  Washington haihusiki kivyovyote na milipuko ya Iran, na wala hakuna dalili zinazothibitisha pia kuhusika Israel katika shambulizi hilo.

Hii ni katika hali ambayo hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililodai kuhusika na tukio hilo la Kerma na hii ni pamoja na kuwa tukio hilo limetokea muda mfupi baada ya mauaji mengine ya kigaidi yaliyofanywa na na utawala huo ghasibu dhidi ya Sayyid Razi Mousavi, mmoja wa washauri wakuu wa kijesi wa Iran nchini Syria, kisha Saleh al-Arouri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas nchini Lebanon. Ni kutokana na matukio hayo, ndipo tuhuma zote zikaelekezwa kwa utawala wa Kizayuni kuwa ndio umekeleza mauaji hayo yote kutokana na utambulisho wake wa kigaidi.

Ni wazi kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni mhimili wa mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo, bado inaendeleza jitihada zake katika uwanja huo, na kamwe vitendo vya kigaidi havijaweza kuizuia kufikia malengo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ahmed Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesisitiza kuhusu shambulio la kigaidi la Kerman kwa kusema: Kitendo hiki cha kigaidi kitafuatiliwa na jibu kali na la haraka kutolewa na vikosi vya kiusalama na kijeshi.