Iran inaitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106860-iran_inaitaka_jamii_ya_kimataifa_kuchukua_hatua_kali_dhidi_ya_ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema jamii ya kimataifa inahitaji kuchukua hatua kali ili kupambana na ugaidi.
(last modified 2026-05-13T14:18:38+00:00 )
Jan 05, 2024 23:29 UTC
  • Iran inaitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali dhidi ya ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema jamii ya kimataifa inahitaji kuchukua hatua kali ili kupambana na ugaidi.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Ali Sabry siku ya Ijumaa, Amir-Abdollahian alipongeza salamu za rambi rambi za nchi hiyo ya Kusini mwa Asia kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran.

Amesema vikosi vya usalama vya Iran vinachunguza kila kitu kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha na kukusanya taarifa kuhusu wahusika.

Hujuma ya kigaidi Januari 3 ilitekelezwa karibu na eneo la kaburi la Shahidi kamanda wa kupambana na ugaidi wa Iran, Luteni Jenerali Qassem Soleimani wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka wa nne wa kuuawa kwake shahidi. Hujuma hiyo ya kigaidi ilisababisha vifo vya watu 89 wakiwemo Wairani 76 na Waafghani 13 na kujeruhi 286, baadhi yao wakiwa katika hali mbaya.

Sabry alimwambia mwenzake wa Iran kwamba Sri Lanka inalaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya Kerman na inasimama pamoja na serikali ya Iran na watu katika mapambano yao dhidi ya ugaidi.

Mazishi ya watu wa Iran waliouawa katika hujuma ya kigaidi mjini Kerman

Siku ya Ijumaa pia, Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani naye pia alilaani  mashambulizi ya umwagaji damu ya kigaidi huko Kerman na kutoa salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Iran.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, mawaziri hao wawili walionya kuhusu athari mbaya za hatua ya kijeshi ya Israel dhidi ya Lebanon na mauaji ya naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas ya Palestina Saleh al-Arouri mjini Beirut katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye kitongoji cha kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo.

Amir-Abdollahian na Al Thani pia walijadili matukio ya hivi karibuni huko Gaza, eneo ambalo limekuwa chini ya mashambulizi ya Israel kwa zaidi ya miezi mitatu. Halikadhalika mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Qatar walijadili pia madai ya Marekani kuhusu meli zinazopitia Mlango-Bahari wa Bab el-Mandeb na Bahari Nyekundu.

Wanadiplomasia hao wakuu wa Iran na Qatar wamesisitiza haja ya kusitishwa mara moja mauaji ya Israel dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza na pia wamepinga mpango wowote kuwahamisha Wapalestina wa Gaza lazima. Aidha wametaka utawala wa Kizayuni wa Israel uondoe mzingiro wake dhidi Gaza na uruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie Wapalestina wa eneo hilo.