Iran yawakamata washukiwa kadhaa wanaohusishwa na hujuma ya kigaidi Kerman
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106864-iran_yawakamata_washukiwa_kadhaa_wanaohusishwa_na_hujuma_ya_kigaidi_kerman
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi ametangaza kukamatwa kwa washukiwa kadhaa wa shambulio la kigaidi la Januari 3 katika mji wa Kerman, ambapo watu 89 waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 285 walijeruhiwa.
(last modified 2024-01-05T23:39:36+00:00 )
Jan 05, 2024 23:39 UTC
  • Iran yawakamata washukiwa kadhaa wanaohusishwa na hujuma ya kigaidi Kerman

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi ametangaza kukamatwa kwa washukiwa kadhaa wa shambulio la kigaidi la Januari 3 katika mji wa Kerman, ambapo watu 89 waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 285 walijeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji huo wa kusini-mashariki siku ya Ijumaa, waziri huyo alisema vikosi vya usalama vya Iran vimepata "taarifa zenye uzito" zinazoelekeza waliko wahusika wa mashambulizi hayo ya kigaidi.

Vahidi alisema vikosi vya usalama vya Iran vina udhibiti kamili wa suala hilo. Amesisitiza kuwa, "Watu wote waliohusika katika tukio la kigaidi bila shaka watatambuliwa na kukamatwa." Siku ya Ijumaa, Wairani walishiriki katika mazishi makubwa ya watu waliouawa shahidi katika milipuko hiyo ya mabomu.

Wairani 76 na Waafghani 13 hadi sasa wamethibitishwa kufariki katika hujuma hiyo ya kigaidi.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi Kerman

Hujuma hiyo ya kigaidi ilifanywa katika kumbukumbu ya kumuenzi Kamanda wa vita dhidi ya ugaidi Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyeuliwa kigaidi katika hujuma ya jeshi katili la  Marekani huko Baghdad Iraq miaka minne iliyopita. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi nchini Iran.

Katika taarifa yake saa chache baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alisema wahusika watakabiliwa na adhabu inayostahiki na majibu makali.

Kundi la magaidi wakufurishaji wa Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi katika taarifa iliyochapishwa kwenye chaneli zao tanzu za Telegram. Daesh imesema wanachama wake wawili walilipua mikanda yao ya vilipuzi katika umati wa watu.