Mtaalamu wa UN alaani vikali hujuma ya kigaidi katika mji wa Kerman
Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran Javaid Rehman amelaani vikali shambulio dhidi ya mjumuiko wa kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa kamanda wa ngazi za juu nchini Iran Shahidi Qassem Soleimani katika mji wa Kerman.
Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR jijini Geneva Uswisi, Rehman amesema wale wote waliohusika na mashambulizi mabaya yaliyotokea siku ya Jumatano nchini Iran na kuua zaidi ya watu 89 lazima wawajibishwe.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: “Mauaji ni mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya maadili ya kimataifa ya haki za binadamu." Aidha ametuma salamu za rambirambi na pole kwa familia za wahanga na wananchi wa Iran.
Wakatio huo huo, Makanisa ya Wakaldayo wa Ashuru ya Tehran na Baraza la Ukhalifa la Waarmenia Wote wa Azerbaijan yametoa taarifa tofauti yakilaani hujuma ya kigaidi huko Kerman.
Katika taarifa hizo, huku yakilaani vikali kitendo hicho cha kigaidi katika kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Hajj Qassem Soleimani, yametoa pole kwa familia za mashahidi na majeruhi katika tukio hilo.
Hujuma hiyo ya kigaidi ilifanywa katika kumbukumbu ya kumuenzi kamanda wa vita dhidi ya ugaidi Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyeuliwa kigaidi katika hujuma ya jeshi katili la Marekani huko Baghdad Iraq miaka minne iliyopita. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi nchini Iran.
Kundi la magaidi wakufurishaji wa Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi katika taarifa iliyochapishwa kwenye chaneli zao tanzu za Telegram. Daesh imesema wanachama wake wawili walilipua mikanda yao ya vilipuzi katika umati wa watu.
Wananchi wa Iran jana Ijumaa walishiriki katika shughuli ya mazishi ya pamoja kwa wahanga wa miripuko miwili ya kigaidi iliyotokea Jumatano katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa nchi huku viongozi wa ngazi za juu nchini wakiahidi kuwasaka magaidi popote walipo.