Magaidi wote waliohusika katika shambulio la Kerman wakamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i106898-magaidi_wote_waliohusika_katika_shambulio_la_kerman_wakamatwa
Magaidi wote waliohusika katika shambulio la kigaidi la hivi karibuni katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran wamekamatwa.
(last modified 2024-01-07T01:00:37+00:00 )
Jan 07, 2024 01:00 UTC
  • Magaidi wote waliohusika katika shambulio la Kerman wakamatwa

Magaidi wote waliohusika katika shambulio la kigaidi la hivi karibuni katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran wamekamatwa.

Mwendesha mashtaka wa jiji hilo Mehdi Bakhshi alifichua habari hizo katika mahojiano ya televisheni siku ya Jumamosi, siku tatu baada ya shambulio hilo la kigaidi.

Amenukuliwa na shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, akisema watu 32 wamekamatwa kuhusiana na hujuma ya kigaidi ya Kerman na wanasailiwa na maafisa wa usalama.

Afisa huyo wa mahakama ameongeza kuwa "mabomu 16 yamegunduliwa katika jimbo lote la Kerman" ambayo nguvu zake za milipuko zilikuwa zaidi ya mabomu yaliyotumiwa katika shambulio la Jumatano.

Kundi la kigaidi la Daesh linaloungwa mkono na Marekani limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi.

Jumatano alasiri, milipuko miwili ya kigaidi ilitokea katikati mwa umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakishiriki marasimu ya kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu,  katika barabara inayoelekea kwenye makaburi ya mashahidi huko Kerman, ambayo ilipelekea kuuawa shahidi watu 89 na kujeruhi wengine 284.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi Kerman

Bakhshi amekanusha uvumi kwamba vilipuzi vilivyotumika wakati wa shambulio hilo viliwekwa kwenye jaa la takataka na kuongeza kuwa milipuko yote miwili ya mabomu ilitekelezwa na magaidi waliokuwa wamejifunga mishipi ya mabomu na kisha kujilipua miongoni wa wananchi. Amesema mmoja wa magaidi hao amabainika kuwa ni raia wa Tajikistan.

Huku akisisitiza kuwa magaidi hawakuweza kutega vilipuzi vyovyote ndani ya makaburi walikozikwa mashahidi, mwendesha mashtaka amesema: "Katika miezi ya hivi karibuni, magaidi 23 wa kundi la kigaidi la Daesh waliokuwa tayari kufanya mashambulizi ya kujiripua wametiwa mbaroni katika jimbo la Kerman."

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ugaidi duniani, na hadi sasa zaidi ya watu na maafisa wake 17,000 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi. Kwa hakika tokea mwanzoni mwa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuvurugwa mfumo wa kistakibari duniani, Iran imekuwa mlengwa mkuu wa chuki na uadui wa maadui, hasa Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao.