Amir Abdollahian: Kuna ulazima wa jamii ya kimataifa kukabiliana ipasavyo na ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, amesitiza ulazima wa kufanyika juhudi kubwa zaidi za jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana ipasavyo na ugaidi.
Hossein Amir Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Catherine Colonna, na kusisitiza kuwa jamiii ya kimataifa inawajibika kupambana na aina zote za ugaidi.
Ameashiria hatua za Ufaransa kuhusu suala la Palestina na kusema: Kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanyika huko Gaza, udharura wa kuchukuliwa hatua za kivitendo za kukomesha mauaji ya raia, kuwezesha operesheni za kutumwa misaada ya kibinadamu, kuzuia mipango ya kuwahamisha kwa lazima wakazi wa Gaza na kuwapa Wapalestina haki ya kujiamulia mustakabali wao kupitia njia ya kidemokrasia, ni hatua madhubuti zaidi ya kumaliza ghasia katika eneo hilo.
Amir Abdollahian ameongeza kuwa: Njia pekee ya kuzuia kupanuka migogoro ya sasa katika eneo la Magharibi mwa Asia na kutengeneza amani ya kudumu ni kutiliwa maanani chanzo cha changamoto zilizopo na pia kuwa na azma ya dhati ya kusaidia kutatua changamoto hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mauaji ya raia, wanawake na watoto zaidi ya 22,000 huko Gaza na kuitaja Marekani na utawala wa Israel kuwa ndiyo wahusika wa mauaji ya halaiki ya hivi sasa huko Palestina. Amesema: "Huwezi kupuuza chanzo cha ukosevu wa utulivu, uvamizi wa Israel na mauaji yake dhidi ya raia kisha ukadai kuwa una wasiwasi juu ya usalama wa Bahari ya Shamu na eneo la Magharibi mwa Asia."
Amir Abdollahian ameongeza kuwa: Usalama wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umefungana na usalama wa eneo hilo, na vita sio suluhisho.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna, amelaani shambulizi la kigaidi la Kerman huko kusini magharibi mwa Iran.
Ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mivutano katika eneo la Asia Magharibi, na kuiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ichukue jukumu la kuzuia kupanuka kwa mgogoro huo.