Jan 20, 2024 04:03 UTC
  • Magaidi kadhaa wa shambulio la Kerman wauawa, baadhi wakamatwa

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imesema vikosi vyake vimefanikiwa kuwaangamiza na kuwatia mbaroni magaidi kadhaa wa shambulio la kigaidi la mapema mwezi huu katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran lililopelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa makumi ya watu.

Katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, wizara hiyo ilisema kuwa, maafisa usalama wa Iran wamewaangamiza magaidi wawili wa hujuma hiyo, sambamba na kuwakamata wengine kadhaa. Miongoni mwa magaidi waliotiwa nguvuni ni Mohammad Imran Tanvir (Abu Imran), mtaalamu wa kuunda mabomu na mmoja wa viongozi wa genge la kigaidi la Daesh-Khorasan.

Taarifa ya Wizara ya Intelijensia ya Iran imeeleza kuwa, vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimefanikiwa kutwaa silaha za zana za magaidi hao, yakiwemo mabomu mawili ya kilo 20, bunduki ya rashasha aina ya US MP4  yenye risasi 278, bunduki aina ya AK-47 yenye risasi 181, maguruneti 7, kamera, vitenzambali 3, nyaya za umeme pamoja na silaha nyinginezo. 

Aidha mapema mwezi huu, Mwendesha Mashtaka wa Kerman, Mehdi Bakhshi alisema watu 32 wamekamatwa kuhusiana na hujuma ya kigaidi ya Kerman na wanasailiwa na maafisa wa usalama.

Jumatatu iliyopita pia, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza kuwa, limevurumisha makombora ya balestiki kulenga ngome za magaidi walioko Syria, waliohusika katika mashambulizi ya hivi karibuni katika miji ya Kerman na Rask ya Iran.

Mashahidi wa shambulio la kigaidi la Kerman

Alasiri ya Januari 3, milipuko miwili ya kigaidi ilitokea katikati mwa umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakishiriki marasimu ya kumbukumbu ya kutimia mwaka wa nne tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu,  katika barabara inayoelekea kwenye makaburi ya mashahidi huko Kerman, ambayo ilipelekea kuuawa shahidi watu 94 na kujeruhi wengine 211.

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) linaloungwa mkono na Marekani lilidai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi mjini Kerman, katika taarifa iliyochapishwa kwenye chaneli zao tanzu za Telegram. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ugaidi duniani, na hadi sasa zaidi ya watu na maafisa wake 17,000 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi. 

Tags