Gharadhi ya Pakistan na Iran ya kuimarisha ushirikiano
Kuimarika kwa uhusiano wa Iran na Pakistan baada ya takribani saa 72 za mvutano kumeonyesha kwa mara nyingine tena kwamba, kuna dhamira kubwa ya pande zote mbili ya kudumisha uhusiano thabiti wa nchi hizi mbili jirani za Kiislamu.
Baada ya shambulio la Iran kwenye makao makuu ya magaidi nchini Pakistan na shambulio kama hilo la Pakistan katika maeneo kadhaa ya mpaka wa Iran, ambayo kwa mujibu wa serikali ya nchi hii yalikuwa makazi ya magaidi wa Pakistan, kivuli cha suutahafahamu kilitanda kwa muda mfupi katika uhusiano mkongwe wa nchi hizi mbili muhimu za Kiislamu, lakini mamlaka nchi hizo mbili zilisisitiza haja ya kuzuia kuongezeka kwa mvutano, na kisha Islamabad ikatangaza kufikiwa makubaliano na Tehran ili kupunguza mvutano katika uhusiano wa pande mbili.
Jumatatu ya juzi Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan zilitoa taarifa ya pamoja inayosema kuwa, kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Pakistan, pande hizo mbili zimekubaliana kuwa mabalozi wa nchi hizo mbili watarejea katika vituo vyao vya kazi ifikapo Januari 26. Pia, kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Jalil Abbas Jilani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hussein Amir Abdollahian atazuru Pakistan Januari 29, 2024.
Kurejeshwa kwa uhusiano wa Iran na Pakistan katika hali ya kawaida kunatimia katika hali ambayo, baadhi ya pande zinazonufaika na mvutano na kufifia uhusiano kati ya Tehran na Islamabad zilikuwa zikijaribu kuzidisha hali ya wasiwasi kwa kulikuza na kuangazia suala la hatua ya kijeshi ya Iran dhidi ya magaidi nchini Pakistan na hivyo kuchochea moto wa fitina katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuichukulia hatua hiyo ya Iran kama utanuaji misuli dhidi ya majirani zake.
Hii ni katika hali ambayo, Iran na Pakistan zina nafasi maalumu kwa kila mmoja katika sera zao za kigeni. Uhusiano wa muda mrefu na imara kati ya pande hizo mbili unarejea nyuma hadi miaka ya mbali sana karibu na siku za mwanzo za uhuru wa Pakistan kutoka India (1947). Mshabaha na mfanano mwingi wa kihistoria, kitamaduni na kidini na kuwepo kwa zaidi ya kilomita 900 za mpaka wa pamoja wa ardhini baina ya nchi hizi mbili ni sababu za kudumu kwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Iran na Pakistan zina utendaji wa pamoja katika masuala muhimu ya kieneo na kimataifa, likiwemo suala la kukabiliana na jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni, na aghalabu zimekuwa zikiunga mkono misimamo ya kila mmoja katika taasisi za kimataifa, jambo ambalo ni sababu nyingine ya mafungamano na nguvu ya uhusiano wa Tehran na Islamabad.
Kwa upande wa biashara pia, ushirikiano wa kuanzisha vituo viwili vya mpakani katika maeneo ya Rimdan-Gabd" na Pishin-Mand na kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano wa kuanzisha masoko sita ya pamoja ya mpakani ni mifano miwili ya azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan ya kukuza ushirikiano katika uga wa kiuchumi.
Pakistan inaweza kukidhi mahitaji ya Iran katika sekta ya kilimo na Iran pia inaweza kudhamini mahitaji ya nishati ya Pakistan; bomba la gesi la Iran-Pakistan (IP) ambalo ni njia ya bei nafuu na salama zaidi ya kusambaza gesi kwa Pakistan, limejengwa na Iran hadi kwenye mpaka wa Pakistan kwa kuzingatia makubaliano ya awali ya pande husika, na sasa ukamilishaji wake unahitajika hatua kutoka upande wa Pakistan.
Suala pekee ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya matatizo katika uhusiano kati ya Iran na Pakistan katika miaka ya nyuma ni kuwepo kwa baadhi ya makundi ya kigaidi hapa nchini na kupanga oparesheni za kigaidi dhidi ya Iran, jambo ambalo limepelekea kuuawa shahidi baadhi ya watu wa Iran na walinzi wa mpakani. Hii ni pamoja na kuwa, usalama wa nchi hizo mbili unategemeana huku ugaidi ukiwa ni hatari ya pamoja kwa Iran na Pakistan. Kwa msingi huo mamlaka za nchi hizo mbili zimeafikiana kuhusu mapambano ya pamoja dhidi ya ugaidi na kuimarisha uhusiano.
Kuhusiana na hili, Nasser Kanani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alisema Jumatatu kuhusu matukio ya hivi karibuni katika uhusiano kati ya Tehran na Islamabad kwamba: Tukio la hivi karibuni halitapunguza nguvu ya uhusiano kati ya Iran na Pakistan. Hivyo mtu asifikirie kwamba, atatumia vibaya anga iliyochafuka kidogo hivi karibuni katika uhusiano wa Tehran na Isalamabad na wala asiwe na tamaa ya hilo.