Feb 08, 2024 03:03 UTC
  • Rais Raisi: Ni haki ya taifa la Iran kunufaikia na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo hapa Tehran na kutilia mkazo wajibu wa kila taifa kufaidika na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani na kwamba ni haki ya taifa la Iran pia kunufaika na nishati hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatano ikiwa ni sehemu ya sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na sambamba na kugusia kuwa ni haki ya wananchi wa Iran kumiliki nishati ya matumizi ya amani ya nyuklia amesema kuwa, fatwa ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu iko wazi kwamba ni haramu kisheria kumiliki silaha za nyuklia hivyo silaha za namna hiyo hazimo kabisa kwenye ratiba za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu.

Amesema, nchi zinazomiliki mabomu ya nyuklia zinafanya njama za kuwanyima wananchi wa Iran haki yao isiyopingika ya kumiliki teknolojia ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na sisi hatuwezi kamwe kukubaliana na jambo kama hilo.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetangaza rasmi mara 15 kwamba Iran haijakwenda kinyume hata kidogo na shughuli za matumizi ya amani za nyuklia, lakini wakala huo na madola ya Magharibi hayaheshimu hata matamshi yao wenyewe.

Sayyid Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, taifa la Iran limeweza kubadilisha vikwazo vya Marekani na Magharibi na kuwa fursa nzuri kwake ya kujiletea maendeleo na kutegemea wataalamu wake wa ndani na kwamba Tehran haijaondoka kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia na haitoondoka, lakini muda wote itaendelea kubainisha kwa uwazi misimamo yake na itapigania kikamilifu haki zake.

Tags