Feb 16, 2024 02:47 UTC
  • Rais Raisi: Uwepo wa maajinabi umelizidishia eneo hili matatizo

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inapinga vikali uwepo wa madola ajinabi katika eneo hili la kistratejia la Asia Magharibi.

Rais Ebrahim Raisi aliyasema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Armenia, Mher Grigoryan na kuongeza kuwa, mielekeo chanya inaweza kutatua matatizo ya eneo hili pasi na kuwahitaji maajinabi.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, uwepo wa madola vamizi Asia Magharibi haujakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuibua taharuki na kudhoofisha usalama wa eneo hili.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, usalama wa eneo hili utaimarishwa tu kupitia ushirikiano wa nchi za eneo, kwani uzoefu unaonyesha kuwa uwepo wa maajinabi unaendelea tu kulizidishia eneo hilii matatizo.

Kadhalika Sayyid Raisi amebainisha kuwa, kuna fursa na uwezekano wa kupanua zaidi uhusiano wa Tehran na Yerevan katika nyuga za siasa, uchumi, biashara, na utamaduni.

Bendera za Iran na Armenia

Katika mazungumzo hayo, Rais wa Iran na Naibu Waziri Mkuu wa Armenia wamefanya mashauriano kuhusu matukio ya kimataifa, kieneo na kuhusu uhusiano wa pande mbili. 

Kwa upande wake,  Naibu Waziri Mkuu wa Armenia, Mher Grigoryan sanjari na kusisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili wa nchi yake na Iran ameeleza kuwa, msimamo wa Yerevan wa kufanya juhudi za kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa na amani haujabadilika. 

Amesema serikali ya Yerevan ina hamu ya kufanya mkutano wa kamisheni ya pamoja ya uchumi na Iran, kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya mataifa haya mawili.

 

 

Tags