Kamanda Salami: Vita vya Gaza vimeifedhehesha Marekani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amesema mauaji ya wanawake, watoto wadogo na raia wengine wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza si kitu chochote kingine ghairi ya aibu na fedheha kwa Marekani.
Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC alisema hayo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, Marekani ina nafasi kubwa na muhimu katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina, na kwamba dunia inatazama na ina ufahamu wa jambo hilo.
Ameeleza bayana kuwa, "Mauaji ya raia wasio na hatia wa Palestina si kitu kingine isipokuwa fedheha isiyokoma katika kipindi chote cha historia ya mwandamu, na yanaashiria kuporomoka Marekani kimaadili, kisiasa, kiutamaduni, kijamii na kijeshi."
Kamanda Salami sanjari na kulaani jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza amesisitiza kuwa, kinachojiri Gaza ni mauaji ya halaiki.
Kamanda huyo wa SEPAH amenukuliwa na IRNA akisema kuwa, matunda yote ya Marekani, nchi za Magharibi, na Wazayuni yamesombwa na operesheni ya wanamuqawama wa Palestina ya Kimbunga cha al-Aqsa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amebainisha kuwa, mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanapasa kuwatanabahisha Waislamu na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
Meja Jenerali Hossein Salami ameongeza kuwa, Marekani inajaribu kukwepa hamaki za walimwengu, kwa kudondosha toka angani eti vifurushi vya misaada kwa wakazi wa Gaza, hicho kikiwa ni kitendo kingine cha hadaa na fedheha kwa Marekani.