Iran yasajili mafanikio 15 ya nyuklia katika sekta ya tiba
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa nchi hii imesajili mafanikio mapya 15 katika uwanja wa matibabu na dawa aina za Radiopharmaceutical.
Muhammad Eslami amesisitiza kuwa dawa hizo za Radiopharmaceutical zilizotengenezwa hapa nchini ni aina ya tiba ambayo huponya uvimbe wa saratani, ikiwa ni pamoja na tezi dume (prostate).
Eslami ameashiria kuzinduliwa mfumo wa plasma jet unaotumika kutibu majeraha, na kuongeza kuwa, taathira za mfumo huo zimeonekana katika maisha ya watu kutokana na ustawi, kupiga hatua na kasi kubwa ya elimu ya teknolojia ya nyuklia katika nyanja zote.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran pia amesema mafanikio 159 ya kisayansi na kiviwanda katika nyanja ya nyuklia yamezinduliwa na kwamba hatua nzuri zimechukuliwa sambamba na kuendeleza miundombinu ya utafiti na kuharakisha mchakato wa kuifanya ya kibiashara sekta ya nyuklia ya Iran ambayo yana athari kubwa kwa usalama wa chakula na mazingira.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashika nafasii ya saba duniani katika ujenzi wa vituo vya tiba ya protoni, ioni ya kaboni na vituo vya miale.