Kiongozi Muadhamu: Ghaza ndiyo kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Ghaza ni suala ambalo haliwezi kufumbiwa macho kwani ndiyo kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutekeleza vizuri majukumu yake kuhusu Ukanda wa Ghaza.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo leo asubuhi wakati alipoonana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo hapa Tehran pamoja na wananchi wa matabaka tofauti kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul Fitr na kuongeza kuwa, Ghaza si suala linaloweza kusahaulika bali ndiyo kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa.
Ameongeza kuwa, nyoyo za mataifa ya dunia hata nyoyo za watu wa mataifa yasiyo ya Waislamu zinaumizwa na dhulma wanayofanyiwa Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza na hilo limethibitishwa na maandamano makubwa ya mfululizo na ambavyo hayajawahi kutokea mfano wake katika mabara ya Afrika, Asia na Ulaya bali hata nchini Marekani kwenyewe ambayo ndiye muungaji mkono mkuu wa utawala katili wa Israel.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi mno wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani) na sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul Fitr kwa taifa la Iran na mataifa yote ya Waislamu duniani amesema kuwa, maandamano makubwa yasiyo na kifani ya Siku ya Kimataifa ya Quds, ni harakati ya kisiasa na kimataifa iliyofanya maajabu duniani.
Pia amesema, kinachotarajiwa kikamilifu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuona nchi za Waislamu zinakata kikamilifu uhusiano wao wa kisiasa na kiuchumi na utawala katili wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, kama kutaitishwa kura ya maoni katika nchi za Waislamu bila ya shaka yoyote wananchi Waislamu wa nchi hizo watatilia mkazo suala hilo hilo la nchi zao kukata mara moja uhusiano wao wote na utawala dhalimu wa Israel.