Apr 22, 2024 02:32 UTC
  • Mufti Mkuu wa Russia: Kiongozi Muadhamu wa Iran anastahiki kupongezwa

Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu ya Russia amesema kuwa, mwito unaotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei wa kuwataka watu wote duniani kuthamini masuala ya kidini na kimaadili unastahiki kupongezwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Mufti Mkuu wa Russia, Sheikh Rawil Ğaynetdin (راویل عین‌الدین) ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Masuala ya Waislamu nchini humo amesema kuwa, juhudi zote za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran zimeelekezwa kwenye kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu na kwa wanadamu wengine duniani na huko ni katika kutekeleza kivitendo amri za Mwenyezi Mungu. 

Sheikh Ğaynetdin (عین‌الدین) pia amesema, msimamo wake huo unawakilisha Waislamu milioni 25 wa Russia na Baraza la Ulama la nchi hiyo kumpongeza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran akimmkhutubu kwa kumwambia: Hakika yako wewe ni shakhsia mkubwa wa Kiislamu unayeheshimika na ni mashuhuri kote duniani. Wewe ni Kiongozi wa kidini na kimaanawi wa wananchi wa Iran ambao wamerithi historia iliyojaa fakhari na ambao ni sehemu muhimu sana katika Ulimwengu wa Kiislamu. 

Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu ya Russia vilevile ameelezea matumaini yake kwamba jitihada kubwa na zinazokubaliwa na Allah zinazofanywa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika kupigania dini tukufu ya Kiislamu na manufaa ya Waislamu wote duniani, zitaandaa mazingira ya kupatikana amani ya kudumu duniani na kulindwa haki za mataifa ya wanyonge yakiwemo ya Waislamu popote pale walipo. 

Tags