Apr 30, 2024 07:49 UTC
  • Iran: Usalama wa Ghuba ya Uajemi utahakikishwa kwa ushiriki tu wa nchi zote za eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema usalama wa Ghuba ya Uajemi utahakikishwa kwa ushiriki tu wa nchi zote za pwani ya ghuba hiyo.

Kwa mujibu wa IRNA, Hossein Amir-Abdollahian, ameeleza hayo katika ujumbe wake kwa kongamano la Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi na kubainisha kuwa usalama wa Ghuba ya Uajemi utahakikishwa tu kwa ushiriki wa nchi zote za pwani yake; na akaongezea kwa kusema, Ghuba ya Uajemi ni ukanda mpana na wa kipekee wa kuziunganisha Ulaya, Afrika, na Asia ya Kusini na KusiniMashariki; na kwa mtazamo wa kimkakati, ni sehemu ya mfumo muhimu wa mawasiliano duniani unaojumuisha Bahari ya Atlantiki, Bahari ya Mediterania, Bahari ya Sham, na Bahari ya Hindi.
Amir-Abdullahian amesema, umuhimu wa Ghuba ya Uajemi kwa upande wa historia, ustaarabu, jiografia, utamaduni na nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa, usafirishaji wa nishati na jiopolitiki hauhitaji ufafanuzi wala maelezo ya kurudia. Kwa sababu hiyo, umuhimu wa ukanda huu wa majini unazingatiwa sana duniani kote.
Hossein Amir-Abdollahian

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, Ghuba ya Uajemi ni jina la milele na ni turathi ya dunia; na maadhimisho yake yanakumbusha siku walipojitoa mhanga watu mashujaa ambao, kwa juhudi zao, walihitimisha uvamizi na ukoloni wa Wareno kwenye pwani ya kusini baada ya miaka mingi.

Jana Jumatatu, tarehe 10 Ordibehesht, 1403 Hijria, sawa na Aprili 29, 2024 iliyosadifiana na kumbukumbu ya kutimuliwa wakoloni wa Kireno katika maji ya kusini mwa Iran mwaka 1622 Miladia, imepewa jina la Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi.
Ghuba ya Uajemi, ambayo ni njia kuu ya baharini, daima imekuwa na nafasi ya kipekee ya kisiasa na leo hii inajulikana kama njia kuu ya kimataifa ya majini ulimwenguni.
Katika miaka ya hivi karibuni, na kwa kuchochewa na Ukoloni wa Magharibi, baadhi ya nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi zimetaka kupotosha jina la Ghuba ya Uajemi; ilhali ukweli ni kwamba tokea tangu na tangu Ghuba ya Uajemi imekuwa ikijulikana kwa jina hilo.
Ukanda huo mpana wa majini uko kusini na kusini magharibi mwa Iran na karibu na mikoa ya Khuzestan, Bushehr na sehemu ya mkoa ya Hormozgan wa Iran, na una mpaka wa pamoja kwa urefu tofauti na nchi saba za Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Iraq, Saudi Arabia, Oman, Qatar na Kuwait.../

 

Tags