Mar 28, 2024 05:50 UTC
  • Msisitizo wa Iran juu ya haki yake katika medani ya gesi ya Arash

Naibu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Sheria, Mohammed Dehghan, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitafumbia jicho kwa hali yoyote ile haki zake katika medani ya pamoja ya gesi ya Arash na haitaruhusu upande wowote kukiuka sheria za kimataifa katika suala hili.

Mnamo 1962, hifadhi kubwa ya gesi iligunduliwa kaskazini mwa maji ya Ghuba ya Uajemi, ambayo kiasi chake kinakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 35 hadi 60 za gesi. Medani hiyo inashirikisha nchi tatu za Iran, Kuwait na Saudi Arabia na inaitwa "Arash" kwa upande wa Iran na "Al-Durra" kwa upande wa Kuwait.

Nchi za Kuweit na Saudi Arabia zilianza uchimbaji wa uchunguzi katika medani ya gesi ya pamoja ya "Arash/Al-Durra" mwaka 2000, jambo ambalo lilifanyika bila idhini ya Iran kama mshirika katika medani hiyo ya pamoja. Hii ni pamoja na kwamba, pande mbili bado zinahitilafiana juu ya kuainisha mpaka wa pamoja wa maji katika eneo hilo, na tofauti hizi ziliibuka tena wakati Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lilipodai katika mkutano wake wa 44 kwamba, medani ya gesi ya Arash ni mali ya Saudi Arabia na Kuwait na kwamba Iran haina haki katika eneo hilo.

Baada tu ya taarifa hiyo, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alieleza masikitiko yake kwa msimamo huo na akasema haukubaliki. Kan'ani alisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo ushirikiano wa kirafiki na wenye kujenga katika uga wa nishati likiwemo eneo la Arash kwa kuzingatia mazungumzo ya pande mbili na serikali ya Kuwait. Kwa hiyo, mwenendo unaozingatia maslahi ya pande zote unaweza kutayarisha uwanja mzuri wa ushirikiano wa kikanda. Hata hivyo, kutokana na mienendo ambayo wakati mwingine si ya kirafiki ya Kuwait na Saudi Arabia, uchimbaji wa gesi eneo la Arash umeibua utata kati ya nchi tatu za Iran, Kuwait na Saudi Arabia.

Ali Zahedi, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "Kuwait na Saudi Arabia, kutokana na dhana potofu zilizonazo kuhusu msimamo wa kieneo wa Iran, zinadhani kwamba zinaweza kuinyima Tehran mamlaka na haki zake katika eneo la gesi la Arash kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, na kulinyakua eneo hilo kwa kutoa madai ya uwongo, jambo ambalo ni njozi batili. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo kamili wa kutetea haki zake katika medani ya gesi ya Arash na inatarajia Kuwait na Saudi Arabia zitaiheshimu haki hizo."

Kumbukumbu za kihistoria ya mazungumzo kati ya Iran na Kuwait katika miongo sita iliyopita juu ya kuainisha mipaka ya maji na ushirikiano katika uchimbaji wa rasilimali ya gesi ya Arash zinaonyesha kuwa pande hizo mbili zimekuwa zikisisitiza suala la kuwepo maelewano na nia njema, na pia zimetambua haki ya kila mmoja wao katika rasilimali hiyo kubwa ya gesi.

Kijiografia, medani ya gesi ya Arash iko kaskazini mwa Ghuba ya Uajemi, suala ambayo lenyewe linathibitisha kuwa ni eneo la pamoja. Hata hivyo, licha ya mazungumzo ya Kuwait na Tehran, hivi karibuni baadhi ya maafisa wa serikali ya Kuwait wamekuwa wakitoa kauli zinazokinzana kuhusu umiliki wa medani ya gesi ya Arash, jambo ambalo linaweza kusababisha mzozo katika mazungumzo yajayo. Hapana shaka yoyote pia kwamba, madola ya kigeni ya nje ya eneo hilo pia yatajaribu kutumia suala hilo kwa maslahi yao wenyewe kupitia propaganda za vyombo vya habari. 

Kuwait na Iran zimetambua haki ya kila mmoja wao katika rasilimali kubwa ya gesi ya Arash.

Ni kwa sababu hiyo ndipo Naibu wa Rais wa Iran akasisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Tehran ingali inaamini kwamba suala hilo linaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo ya pande mbili na Kuwait lakini haitaruhusu nchi hiyo au nchi nyingine yoyote kuchukua hatua kinyume na kanuni na kisheria vya kimataifa kwa kutumia rasilimali hiyo kwa upande mmoja bila kujali maslahi ya Iran.

Tags