Apr 25, 2024 10:01 UTC
  • Spika wa zamani wa Marekani: Netanyahu anapaswa ajiuzulu, amekwamisha amani kwa miaka kadhaa

Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi amesema, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni kizuizi cha kupatikana amani Ghaza na anapaswa ajiuzulu.

Pelosi ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Raidió Teilifís Éireann ya Ireland wakati wa ziara yake nchini humo.

Spika huyo wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Marekani ameikosoa Israel pia kwa aina ya jibu la kijeshi ililotoa kwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa Oktoba 7 na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas dhidi ya vituo vya kijeshi na vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel. 

Katika mahojiano hayo Pelosi amesema: "Tunatambua haki ya Israel ya kujihami, lakini tunakataa sera na hatua ya Netanyahu, ni mbaya sana. Kuna baya zaidi kuliko alichofanya katika jibu alilotoa?"

Netanyahu

"Anapaswa ajiuzulu, ni yeye hasa anayepaswa kuwajibika", amesisitiza Spika huyo wa zamani wa Bunge la Marekani.

Alipoulizwa kama Netanyahu ni "kizuizi" cha amani, Pelosi alijibu: "amekuwa kwa miaka mingi," akiongeza kwamba hajui kama kiongozi huyo wa Israel "anaogopa amani, hawezi kuisimamia amani, au hataki amani.”

Nancy Pelosi ameendelea kueleza kwamba, Netanyahu amekuwa "kizuizi kwa suluhisho la serikali mbili, na akasema "natilia mkazo neno 'suluhisho'."

Mapema mwezi huu, spika huyo wa zamani wa bunge la Marekani alijiunga na zaidi ya wajumbe 30 wa bunge la nchi hiyo ambao walitia saini barua ya kuwataka Rais Joe Biden na Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken wasitishe kuipelekea silaha Israel.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, tayari serikali ya Washington imeshaidhinisha kuupatia utawala wa Kizayuni fungu la msaada wa dola bilioni 26 ili uendeleze vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghaza, ambao idadi yao imeshapindukia 34 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.../

 

Tags