Apr 26, 2024 10:49 UTC
  • Mvua kali zabomoa ukuta mbovu wa jela Nigeria na kuwezesha wafungwa zaidi ya 100 kutoroka

Zaidi ya wafungwa 100 wametoroka jela baada ya mvua kali kubomoa ukuta mbovu wa jela hiyo iliyoko karibu na mji mkuu wa Nigeria Abuja.

Mamlaka husika za magereza nchini Nigeria zimetangaza kuwa wafungwa 118 walitoroka kwenye Gereza la Suleja, lakini 10 kati yao tayari wamekamatwa huku msako mkali ukiendelea kuwatafuta waliosalia.
 
Taarifa kuhusu utambulisho wa wafungwa waliotoroka bado hazijawekwa wazi, jambo linalozusha wasiwasi kuhusu hatari zinazoweza kutokea kwa usalama wa umma. Hata hivyo, uongozi wa magereza umesema, hatua zinachukuliwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kukabiliana na hali hiyo na kuwataka wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku bila ya wasiwasi.
"Kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, hadi sasa tumewakamata tena wafungwa 10 waliokuwa wakitoroka na kuwaweka chini ya ulinzi, huku tukiwa katika msako mkali wa kukamata wengine", imesema Mamlaka ya Magereza ya Abuja.

Tukio hilo limetoa picha ya changamoto kubwa zinazoukabili mfumo wa magereza wa Nigeria, hasa hali mbaya ya vituo vingi vya kuwekea wahalifu. Magereza kama la Suleja yaliyojengwa tangu enzi za ukoloni yamechakaa na kuwa hatarini kubomoka, na hivyo kuzidisha hatari za kiusalama.

 
Tukio hilo la utorokaji wafungwa zaidi ya 100 katika jela moja linafananishwa na jengine lililotokea miaka miwili iliyopita, ambapo zaidi ya wafungwa 400 waliwezeshwa kutoroka kufuatia shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika gereza jengine lililoko mjini Abuja pia. Tukio hilo lilisababisha maafa ikiwa ni pamoja na kuuawa wafungwa wanne, mlinzi na washambuliaji wengi.
 
Tangu mwaka 2020, zaidi ya wafungwa 5,000 wametoroka jela nchini Nigeria katika matukio ya mashambulio dhidi ya magereza, jambo linalodhihirisha changamoto zinazoendelea kuukabili mfumo wa magereza katika kuhakikisha ulinzi madhubuti unawekwa katika jela za nchi hiyo.../
 

Tags