Mar 25, 2024 11:22 UTC
  • 17 wapoteza maisha wakigombania chakula cha msaada Nigeria

Kwa akali watu 17 wameaga dunia katika mkanyagano wa kugombania chakula cha msaada nchini Nigeria.

Ahmed Wakil, Msemaji wa Polisi katika Jimbo la Bauchi amesema mbali na watu 17 kupoteza maisha, wengine zaidi ya 30 wakiwemo watoto wadogo na wanawake wamejeruhiwa kwenye mkasa huo uliotokea jana Jumapili jijini Bauchi, kaskazini mashariki mwa nchi.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Ahmed Sani, ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, mkanyangano huo ulitokea baada ya mamia ya wanawake na vijana kugombania chakula cha msaada na sadaka. Aidha wanawake wawili wajawazito wameripotiwa kujifungua kutokana na uzito wa mkanyagano huo.

Shirika la habari la Iran Press limeandika kuwa, wakazi hao wa Bauchi walikuwa wamekusanyika katika ofisi za mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Alhaji Yakubu Maishanu Shafa kupokea chakula cha msaada pamoja na Naira 10,000 (dola 7) alizokuwa akimpa kila mmoja.

Nigeria, mbali na mgogoro wa kiuchumi, inasumbuliwa pia changamoto za kiusalama

Shuhuda mwingine, Hajiya Jamila anasema alishuhudia maiti nne katika mkanyangano huo, na pia watu saba waliozirai kwa kukosa hewa wakati wa tukio hilo.

Haya yanajiri siku mbili baada ya wanachuo kadhaa kujeruhiwa katika mkanyagano mwigine wa kugombania chakula cha msaada katika Chuo Kikuu kimoja katika jimbo la kaskazini la Nasarawa.

Ripoti ya wiki iliyopita ya Shirika la Takwimu za Taifa (NBS) inasema kuwa, Nigeria inashuhudia mgogoro wa chakula na uchumi uliodorora, huku mfumuko wa bei za bidhaa ukifikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha asilimia 31.7 mwezi Februari mwaka huu.

Tags