May 05, 2024 07:38 UTC
  • Maandamano yanaendelea kote duniani kulaani hujuma ya Israel dhidi ya Gaza

Miji ya nchi mbalimbali duniani jana Jumamosi ilishuhudia maandamano ya kulaani uvamizi na vita vya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina, ambapo washiriki wametoa wito wa kusitishwa mapigano haraka iwezekanavyo.

Waandamanaji hao wameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha vita vya Israel dhidi ya Gaza na kutuma misaada ya kibinadamu kwa watu wa Palestina.

Mamia ya wanaharakati walifanya maandamano jana Jumamosi mbele ya Chuo Kikuu cha London College wakionyesha mshikamano wao na wanafunzi wanaofanya mgomo ndani ya kampasi ya chuo hicho, wakipinga vita vya Israel huko Gaza na kutaka chuo hicho kijitenge na taasisi na makampuni yanayoshirikiana na utawala uvamizi wa Israel.

Kaskazini mwa Uingereza pia, kumeshuhudiwa maandamano makubwa katika mitaa ya Manchester ambako waandamanaji walipiga ngoma na kutoa kaulimbiu zinazotaka kukombolewa Palestina.

Huko Paris, Wafaransa waliandamana jana wakitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza,  na kusisitiza haja ya kuiwajibisha Israel kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.

Maandamano dhidi ya Israel katika nchi za Ulaya

Waandamanaji hao wamezituhumu nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kuwa zinashirikiana na Israel na kuipatia ulinzi wa kisiasa ili kukwepa adhabu na kuwajibishwa.

Maandamano kama hayo yalifanyika pia katika mji mkuu wa Austria, Vienna, Berlin nchini Ujerumani, Stockholm nchini Sweden, Odense huko Denmark na New York Marekani ambako washiriki wametoa wito wa kusitishwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza.