May 06, 2024 07:47 UTC
  • Iran yatathmini njia za kuimarisha uhusiano wake na Tunisia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inachunguza njia na majukwaa ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili kati yake na Tunisia.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumapili akiwa njiani kurejea hapa nchini akitokea mji mkuu wa Gambia, Banjul, alikoenda kushiriki mkutano wa 15 wa kila mwaka wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Amir-Abdollahian amekutana na kufanya mazungumzo mafupi na afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Tunisia aliposimama kidogo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Tunis, mji mkuu wa Tunisia.

Abdollahian katika mazungumzo yake hayo na Mkurugenzi wa Kieneo anayesimamia Hafla Rasmi za Taifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ameeleza kuwa, serikali ya Rais Ebrahim Raisi ina hamu ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na nchi za Afrika na za Kiarabu ikiwemo Tunisia.

Wawili hao wamesisitiza kwamba serikali za Iran na Tunisia zimeazimia kuimarisha uhusiano wa pande zote, na kwamba pande mbili hizo zinatathmini njia za kuboresha zaidi ushirikiano wao.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran mjini Tunis, Mir Massoud Hosseinian pamoja na maafisa wengine wanaofanyakazi katika ubalozi huo.

 

Tags