Araqchi amwambia Guterres: Simamisheni uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137426-araqchi_amwambia_guterres_simamisheni_uchokozi_wa_marekani_na_israel_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Matatizo ya usafirishaji wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni matokeo ya vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kila nchi au shirika la kimataifa linalojali amani na usalama lazima lilaani uhalifu wa tawala hizo mbili na kutoa wito wa kukomeshwa uchokozi wao wa kijeshi dhidi ya taifa la Iran."
(last modified 2026-03-17T08:43:36+00:00 )
Mar 17, 2026 08:43 UTC
  • Araqchi na Guterres
    Araqchi na Guterres

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Matatizo ya usafirishaji wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni matokeo ya vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kila nchi au shirika la kimataifa linalojali amani na usalama lazima lilaani uhalifu wa tawala hizo mbili na kutoa wito wa kukomeshwa uchokozi wao wa kijeshi dhidi ya taifa la Iran."

Sayyid Abbas Araqchi ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambapo pande hizo mbili zimejadili na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Magharib mwa Asia na uchokozi wa kijeshi unaoendelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, na vilevile hali ya mambo nchini Lebanon.

Akizungumzia ukiukwaji mkubwa wa kanuni na sheria za msingi za Hati ya Umoja wa Mataifa kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha wajibu wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa kulaani vikali na waziwazi uchokozi huo na kuwawajibisha wachokozi kwa mujibu wa Sura ya Saba ya hati hiyo.

Araqchi ameitaka jamii ya kimataifa iangalie chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi na Mlango-Bahari wa Hormuz, yaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel, na akasema: Hali katika Mlango-Bahari wa Hormuz haiwezi kutatuliwa bila kuzingatia hali jumla katika eneo hilo, kwa sababu mkwamo wa safari za meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni matokeo ya vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni, na kila nchi au taasisi ya kimataifa inayojali amani na usalama lazima ilaani uhalifu wa tawala hizi mbili na kutaka kukomeshwa uchokozi wao wa kijeshi dhidi ya taifa la Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amelaani uchokozi wa kikatili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na mauaji ya mamia ya watu nchini humo, akisisitiza: "Kufumbiwa macho na kunyamaziwa kimya ukiukaji wa sheria na jinai za Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na dhidi ya nchi za eneo la Asia Magharibi kutaushajiisha utawala huo kuendeleza uvamizi wake na kuzidisha ukosefu wa usalama katika kanda hii na dunia."

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea maoni yake kuhusu hali ya sasa katika eneo la Ghuba ya Uajemi, eneo la Asia Magharibi na usalama wa baharini.