Apr 26, 2024 08:10 UTC
  • Rais Raisi: Kuna irada ya kuimarisha uhusiano wa Afrika na Iran

Raisi Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuna irada baina ya Iran na Afrika kuimarisha na kustawisha uhusiano wa kibiashara.

Rais wa Iran ameyasema hayo leo asubuhi jijini Tehran alipohutubu katika Kikao cha Pili cha Ushirikiano wa Iran na Afrika. Rais Raisi amesema kikao cha leo ni ishara kuwa pande mbili zina hamu ya kupanua uhisiano wao.

Aidha amesema hatua ya Wizara ya Biashara ya Iran ya kuandaa kikao hicho ni muhimu katika kuwezesha Waafrika kufahamu uwezo wa Iran na Wairani pia kufahamu uwezo wa Afrika.

Rais Raisi amesema pamoja na kuwepo vikwazo, Iran imeweza kupata maendeleo makubwa katika sekta ya teknolojia za kisasa na iko tayari kushirikiana na Afrika katika sekta hiyo.

Amesema tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA) muasisis wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano na Afrika na hivi sasa pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anatilia mkazo ustawi wa ushirikiano na mataifa ya Afrika.

Akiendelea na hotuba yake, Raisi amesema nchi za Magharibi zinalenga kupora utajiri wa Afrika na kuongeza kuwa historia ya Afrika imeonyesha namna Wamagharibi hawajawa ne lengo jingine isipokuwa uporaji. Ameongeza kuwa Iran inataka kuwa na uhusiano na Afrika kwa ajili ya maslahi ya bara Afrika.

Mjumbe wa Umoja wa Afrika Patrick Lalande akihutubu katika kikao cha Iran na Afrika jijini Tehran

Amesema lengo la Iran ni kuliwezesha bara la Afrika kufaidika na utajiri wake wa mali asili kama vile madini. Aidha amesema Iran iko tayari kushirikkiana na Afrika katika sekta za kilimo kwa faida ya pande mbli. Hali kadhalika Rais Raisi amebainisha kuwa Iran itazisaidia nchi za Afrika kustawi kiviwanda. Mbali na hayo Rais wa Iran amesema wataalamu wa Iran wanaweza kushirikiana na wenzao wa Afrika katika miradi ya maendeleo barani humo.

Rais wa Iran amesema ili kuondoa vizingiti katika uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afrika kuna haja ya kufungua njia za usafiri zikiwemo za anga na bahari. Hali kadhalika amesema kadhia ya mabadilishano ya kifedha ni muhimu katika kurahisisha biashara baina ya Iran na Afrika na hivyo changamoto zilizopo zinapaswa kutatuliwa haraka.

Akiashiria safari yake barani Afrika na mikutano yake na viongozi wa Afrika, amesema aghalabu ya nchi za Afrika zina hamu kubwa ya kuwa na uhusiano wa karibu na Iran.

 

Tags