Apr 27, 2024 02:35 UTC
  • Ukosoaji wa Amnesty International kwa njama za Marekani za kuficha jinai za Israel Gaza

Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International, ameonya kuhusu kuendelea kwa ukiukaji wa haki za binadamu huko Gaza na kutangaza kuwa: Marekani inazuia kutuhumiwa Israel kwa kukiuka haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza.

Callamard alisisitiza Jumatano iliyopita kwamba, katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Marekani imezidisha hatua za kuwalinda na kuwakingia kifua viongozi ya Israel dhidi ya kufunguliwa mashtaka kwa kufanya ukiukaji wa haki za binadamu huko Gaza. Aidha amesema, hatua ya Marekani ya kupigia kura ya turufu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Gaza mara 3 hususan kuzuia kwake usitishaji vita huko Gaza imeifanya nafasi ya Baraza la Usalama kutokuwa na maana yoyote.

Sisitizo la Amnesty International kuhusu njama za Marekani za kuficha jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza na pia kuzuia utawala huo kutuhumiwa kukiuka haki za binadamu, kwa mara nyingine tena limefichua undumakuwili na unafiki wa Washington katika uga wa haki za binadamu. Suala la undumakuwili wa nchi za Magharibi hususan Marekani katika uga wa haki za binadamu limekuwa likiibuliwa mara nyingi na nchi zinazopinga satwa na ubeberu wa Magharibi kama Iran na pia wapinzani wa nchi za Magharibi, kama vile China na Russia.

Ijapokuwa dhana ya haki za binadamu inakubalika katika ngazi ya kimataifa na katika jamii ya kimataifa, lakini kwa kuangalia mitazamo, misimamo na utendaji wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani inabainika bayana kuwa Wamagharibi wanayo tafsiri yao mahususi na yenye ukomo ya dhana hii ya kimsingi na yenye mipaka. Wanalitazama suala hili kwa kuzingatia maslahi yao na washirika wao.

Kwa maneno mengine ni kuwa, kila mara madola haya na washirika wao kama vile Israel yanapokiuka haki za binadamu, hilo hupuuzwa kirahisi, huku hatua shadidi na kali zikichukuliwa dhidi ya madai tu ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi zingine, hasa nchi zinazopinga ubeberu na ubabe wa madola ya Magharibi.

Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, haki za binadamu zimekuwa wenzo na chombo cha Wamagharibi cha kuendeshea propaganda na vita vya kisaikolojia dhidi ya nchi zinazopinga hegemonia na mamlaka ya amri ya madola ya Magharibi. Mfano wa wazi wa hili ni kuishutumu Russia kwa kukiuka haki za binadamu na kufanya uhalifu wa kivita huko Ukraine, na hata kutolewa hati ya kukamatwa Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Hii ni katika hali ambayo, daima Marekani imekuwa ikizuia kulaaniwa au takwa la kuchunguzwa jinai nyingi na mtawalia za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na mashambulizi mengi dhidi ya nyumba, shule, hospitali, mashamba na mauaji ya kinyama ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika kipindi cha miezi saba iliyopita tangu kuanza vita vya Gaza, licha ya kuuawa shahidi takriban watu 35,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, lakini Marekani sio tu kwamba, haichukui hatua yoyote dhidi ya Tel Aviv, bali pia inapinga kuchunguzwa kwa jinai hizo katika taasisi za kimataifa za mahakama. Fauka ya hayo, Washington imezuia kutolewa taarifa au kuidhinishwa maazimio dhidi ya vitendo hivyo vya jinai katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na jambo hilo limepelekea kupata kiburi utawala wa Kizayuni cha kutekeleza jinai zaidi dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International,

 

Ingawa jinai za utawala wa Kizayuni hususan mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza na vile vile utumiaji silaha ya njaa katika eneo hilo ni mambo ambayo yamethibiti wazi, lakini Marekani inazuia kulaaniwa utawala huo katika taasisi za kimataifa na kupinga kwa nguvu zote kufanyika uchunguzi wa uhalifu huu katika taasisi za kimataifa za mahakama kama vile Mahakama ya Kimataifa ya ya Jinai. Baada ya Afrika Kusini kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kukiuka Mkataba wa Geneva dhidi ya Mauaji ya Kimbari (1948), Ikulu ya White House ilitangaza waziwazi upinzani wake kwa hatua hii.

Hapana shaka kuwa, Marekani ikiwa mfuasi na mtetezi mkuu wa Israel, ambayo hivi karibuni imetenga dola bilioni 26 za misaada ya kijeshi na silaha, kamwe haitaruhusu jambo kama hilo. Hata hivyo ushahidi usio na shaka kuhusu mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza umezidisha mashinikizo ya kimataifa ya kutolewa waranti wa kukamatwa maafisa wakuu wa Kizayuni kwa kutenda jinai za kivita huko Palestina.

Tags